Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limemtoza faini ya Dola za Marekani 200,000 Rais wa Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT), Samuel Eto’o, kwa ukiukaji wa maadili, lakini likakosa ushahidi wa kutosha kuendelea na mashtaka yanayohusiana na madai ya upangaji wa matokeo.
CAF lilianzisha uchunguzi kuhusu mwenendo wa Eto’o mwezi Agosti mwaka jana baada ya kupokea “taarifa zilizoandikwa na wadau kadhaa wa soka wa Cameroon”.
Jopo la nidhamu la CAF liligundua katika uchunguzi wake kwamba Mwanasoka Bora huyo wa Afrika mara nne “amekiuka kwa kiasi kikubwa kanuni za maadili, uadilifu na uanamichezo” za CAF kwa kutia saini mkataba wa kuwa balozi wa kampuni ya kamari ya 1XBET.
Mawakili wa Eto’o wamesema watakata rufaa kupinga hukumu hiyo.
1XBET inadhamini vitengo viwili vya juu vya kandanda ya kulipwa ya wanaume nchini Cameroon na upande wa kimataifa wa wanaume na wanawake, huku kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), zikisema kuwa watu walio chini ya kanuni zake hawaruhusiwi kujihusisha na kamari.
Julai mwaka jana, kundi linalowakilisha vilabu vya wachezaji wasiocheza soka nchini Cameroon lilimtaka Eto’o kujiuzulu, likieleza wasiwasi wao juu ya uhusiano wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 43 na 1XBET na kuendelea kuongoza Shirikisho la Soka la Cameroon.
Wakati Eto’o amepatikana na hatia ya kukiuka sheria za CAF kimaadili, ameepuka adhabu inayohusiana na upangaji wa matokeo, huku jopo la nidhamu likisema hakuna uthibitisho wa kutosha.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona, ​​Inter Milan na Chelsea alikuwa anachunguzwa pamoja na Valentine Nkwain, Rais wa klabu mpya iliyopandishwa daraja ya Victoria United, kufuatia mazungumzo ya simu ya wawili hao yaliyokuwa yakijadili kurejea kwa Victoria kwenye Ligi Kuu kabla ya kuhakikishiwa kupanda daraja.
Wote wawili hapo awali walikanusha kuhusika katika njama zozote za kuchakachua matokeo.