Rais wa Marekani, Joe Biden amesema ni “Mungu Mwenyezi” pekee ndiye anayeweza kumshawishi kusitisha azma yake ya kugombea tena urais wa nchi hiyo.
Akizungumza katika mahojiano na ABC News, Biden pia ameeleza kukataa kufanya vipimo vya akili na utambuzi (cognitive test) na kuweka matokeo hadharani ili kuwahakikishia wapiga kura kwamba yuko sawa kuhudumu kwa muhula mwingine.
“Nina kipimo cha utambuzi kila siku. Kila siku nina kipimo hicho – kila kitu ninachofanya (ni kipimo),” amemwaambia George Stephanopoulos katika mahojiano.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 81 kwa mara nyingine amekataa wazo lililotolewa na baadhi ya maofisa wa chama chake cha Demokrati pamoja na wafadhili, kwamba anapaswa kujiweka kando na kupisha damu changa baada ya kushindwa kufanya vizuri kwenye mdahalo baina yake na mgombea wa Republican, Donald Trump wiki iliyopita.
Wakati wote wa mahojiano, Stephanopoulos alimbana rais juu ya uwezo wake wa kuhudumu kwa muhula mwingine na hasa akijielekeza kwenye umri na kilichojitokeza kwenye mdahalo ambapo alikuwa anababaika kujibu baadhi ya maswali.
“Sidhani kama kuna mtu aliyefaa zaidi kuwa rais kwa sasa au kushinda kinyang’anyiro hiki kuliko mimi,” Biden amesema, na kujiaumu kwa kutofanya vizuri kwenye mdahalo kutokana na kile anachosema kwamba ni uchovu wa safari na baridi na si vinginevyo.