Stroke au kiharusi
ni tatizo linalotokea ghafla kwenye ubongo ambapo mtiririko wa damu kwenye eneo fulani la ubongo husitishwa ghafla au kupungua sana hivyo kusababisha eneo hilo la ubongo kukosa damu na virutubishi muhimu na seli za eneo hilo kuanza kufa. Hili linaweza kutokea pale mishipa ya damu ya kuelekea kwenye eneo hilo ikiziba au mishipa ndani ya ubongo katika eneo hilo kupasuka. Seli za ubongo za eneo hilo zikianza kufa kwa kukosa damu, shughuli zote zinazoendeshwa na eneo hilo la ubongo husimama kwa mfano kumbukumbu au misuli.
NB
Kiharusi ni ugonjwa wa dharura hivyo tiba inatakiwa ipatikane mapema iwezekanavyo. Kimsingi kiharusi huweza kumpata mtu ye yote wakati wowote.
AINA ZA KIHARUSI
Kuna aina tatu za stroke; ischemic, hemorrhagic na TIA. Kundi la watu lililo kwenye hatari kubwa zaidi ya kuupata ugonjwa huu ni lile la watu wenye miili mikubwa, umri zaidi ya miaka 55, wenye historia ya ugonjwa huu kwenye familia zao, ambao hawafanyi mazoezi , wanaokunywa sana pombe au kutumia madawa haramu.
Kiharusi Husababishwa Na Nini?
Kila moja ya aina za stroke hapo juu inasababishwa na vitu tofauti.
1)Ischemic strokes, ndiyo aina ya stroke inayowaathiri watu wengi zaidi, asilimia 85 ya wagonjwa wa stroke hupatwa na aina hii ya stroke. Aina hii ya stroke husababishwa na kuziba kwa ateri (mishipa ya kusafirisha damu safi) zinazoelekea kwenye ubongo au kusinyaa kwa mishipa hiyo, hivyo kusababisha hali inayoitwa ischemia (upungufu mkubwa wa mtiririko wa damu).
Kuziba kwa mishipa ya damu hutokea baada ya damu kuganda ndani ya ateri zinazoeleka kwenye ubongo au katika maeneo ya mbali zaidi na kusukumwa kwenye mishipa yenye kipenyo kidogo ndani ya ubongo. Mishipa hii inaweza kuzibwa pia na mafuta yaliyoganda ndani ya ateri (plaque).
2)Hemorrhagic strokes, husababishwa na ateri ndani ya ubongo kuvuja damu au kupasuka. Damu hii iliyovuja huleta mgandamizo kwenye seli za ubongo na kuziharibu. Kupasuka kwa mishipa ya damu husababishwa na hypertension, trauma au dawa zinazofanya mishipa hii ya damu kupungua unene wake
3)Transient ischemic attack (TIA), hii ni tofauti na aina hizo mbili za stroke hapo juu kwani hapa mtiririko wa damu kuelekea kwenye ubongo huvurugwa kwa muda mfupi kwa sababu zile zile tulizozitaja hapo juu tulipozungumzia ischemic strokes. Stroke ya aina hii ni ishara ya kutokea strokes nyingine baadaye kama hatua zinazostahili hazitachukuliwa.
Dalili Za Kiharusi (Stroke)
Ugonjwa wa stroke humpata mtu ghafla na dalili hutokea kwa muda mfupi sana. Dalili kuu za ugonjwa huu ni:
- Kuchanganyikiwa, mtu akipata shida ya kuongea na kuelewa anachoambiwa
- Maumivu ya kichwa yanakwenda pamoja na kupoteza fahamu kwa vipindi na kutapika
- Ganzi katika viungo vya uso, mkono na mguu na hasa vikiwa vya upande mmoja wa mwili
- Kupata shida ya kuona kwa jicho moja au yote
- Kupata shida ya kutembea vikichanganyika na kizunguzungu na kukosa mpangilio wa matendo ya mwili
ATHARI ZA KIHARUSI zinaweza kuwa ni za muda mrefu. Kulingana na muda uliopita kabla ya kuugundua na kuutibu ugonjwa huu,
mtu anaweza kupata ulemavu wa muda mfupi au wa kudumu. Pamoja na madhara ya stroke kama yalivyoorodheshwa hapo juu,
mgonjwa wa stroke anaweza pia kupata yafuatayo:
- Msongo wa mawazo
- Maumivu kwenye mikono na miguu yanayoongozeka baada ya viungo hivyo kufanya kazi au kutokea mabadiliko ya hali ya hewa.
- Kupooza au udhaifu wa upande mmoja wa mwili
- Kupata shida katika kufanya matendo ya kuonyesha hisia za mwili
- Kushindwa kumudu matumizi ya kibofu cha mkojo au viungo vya njia ya haja kubwa
TIBA ZA STROKE NA NAMNA YA KUZUIA STROKE
Kwa vile aina kuu mbili za stroke, ischemic na hemorrhagic, kila moja ina chanzo kilicho tofauti, kila moja inahitaji tiba iliyo tofauti na ya aina nyingine. Ni sharti kujua kwa uhakika ni aina gani ya stroke iliyotambuliwa kwani tiba ya stroke ya aina moja inaweza kuwa na madhara kwa stroke ya aina nyingine.
1)TIBA KWA ISCHEMIA STROKE: Ischemic strokes hutokea pale mishipa ya damu inapoziba au kupungua kipenyo hivyo tiba ya tatizo hili ni kuhakikisha damu ya kutosha inaufikia ubongo. Tiba huanza kwa kotoa dawa za kuyeyusha damu au mafuta yaliyoganda na kuzuia hali hiyo isitokee tena.
2)TIBA KWA HEMORRHAGIC STROKE: Stroke ya aina hii hutokea pale damu inapovuja ndani ya ubongo hivyo tiba yake italenga katika kuzuia damu isiendelee kuvuja na kupunguza mgandamizo wa damu iliyovuja juu ya ubongo. Tiba huanza kwa kutoa dawa za kupunguza mgandamizo kwenye ubongo, kupunguza msukumo wa damu kwa ujumla na kuzuia kusinyaa kwa ghafla kwa mishipa ya damu.
ILI KUJILINDA NA STROKE AU KUZUIA STROKE YAFUATAYO YANAWEZA KUFANYWA:
- Kutotumia madawa haramu
- Kula chakula chenye mboga na matunda kwa wingi na chenye cholesterol kidogo
- Kufanya mazoezi kila wakati
- Kuhakikisha unadhibiti blood pressure
- Kuhakikisha unadhibiti kiwango cha sukari mwilini
- Kuwa una uzito unaofaa
- Kunywa pombe kwa kadri au kuacha kabisa
- Kuacha kuvuta sigara