Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa barabara ya Malagarasi – Uvinza (kilometa 51.1) kwa kiwango cha lami ifikapo Machi 2025 kama ilivyopangwa.
Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo akiwa ziarani mkoani Kigoma. Amewasihi viongozi na watendaji kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi huo ili barabara hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuwawezesha wananchi kushiriki vema shughuli za kiuchumi na ujenzi wa Taifa.
Amesema barabara hiyo ni kiungo muhimu cha uchumi na kinachowezesha wananchi kufanya biashara baina yao na nchi za jirani.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kupooza umeme wa msongo wa Kv 132 kilichopo Kijiji cha Nguruka Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma na kuipongeza Wizara ya Nishati kwa maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho ambao umefikia asilimia 95.
Amesema serikali imedhamiria kuufungua Mkoa wa Kigoma ikiwemo upatikanaji wa umeme nafuu ili kuweza kuvutia zaidi wawekezaji. Ameongeza kwamba kuingizwa katika gridi ya Taifa Mkoa wa Kigoma ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba kama ilivyoahidiwa na Wizara ya Nishati kutawezesha wananchi kutumia fursa ya umeme wa uhakika kujiletea maendeleo.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuongeza jitihada katika kulinda mazingira ikiwemo kujielekeza katika kupanda miti na kuzuia uchomaji moto wa misitu.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.