Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amewasihi wananchi wa Kigoma kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi bora.
Dkt. Mpango ametoa wito huo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Uvinza akiwa ziarani mkoani Kigoma.
Aidha amewasihi wananchi hao kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika kutoa maoni kwenye mchakato wa uandaaji wa Dira ya Taifa 2050 unaoendelea.
Vilevile Makamu wa Rais ametoa rai kwa wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kuweka mkazo katika kuhakikisha watoto wanapata elimu ikiwemo kufuatilia mienendo yao mashuleni.
Amesema Taifa lolote ili liweze kupata maendeleo linahitaji watu waliosoma na kwamba kwenye elimu ndimo watatoka viongozi na wafanyakazi bora.
Pia Makamu wa Rais ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kigoma kufanya mazungumzo na mkandarasi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) katika kipande cha Uvinza ili aweze kuwaruhusu wananchi wenye vitambulisho mbadala vinavyowatambulisha kuwa Watanzania kufanya kazi katika mradi huo wakati Wizara ya Mambo ya Ndani ikishughulikia upatikanaji wa vitambulisho vyao vya Taifa.
Vilevile amewaagiza viongozi wa wilaya hiyo kusimamia kikamilifu urejereshaji wa uoto wa asili katika wilaya hiyo ikiwemo kupanda miti na kuisimamia kuhakikisha inaota.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amezungumza na wananchi wa eneo la Kazuramimba ambapo ameiagiza Wizara ya Maji kuhakikisha inakamilisha mradi wa maji uliopo katika eneo hilo ifikapo mwezi Agosti mwaka huu ili kuwaondolea changamoto ya maji wanayokutana nayo wananchi.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara mkoani Kigoma ambapo anakagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi.