Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limemkamata na kumuhoji kwa kina Mussa Khamis Bakari maarufu Buda (30) Wakala wa forodha na Mkazi wa Temeke kwa tuhuma za mauaji ya Abdallah Twahir Selemani ambaye alikuwa Rafiki yake na baada ya kumuua alifanikiwa kuiba pesa za Marehemu Tsh. milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya huyo Rafiki yake.
Akiongea leo July 11,2024 Kamanda Kanda Maalum ya Polisi Dar es salaam, SACP Muliro Jumanne Muliro amesema “May 01, 2024 majira ya saa 10:20 asubuhi huko maeneo ya Mbutu Kichangani, Kigamboni pembezoni mwa barabara itokayo Cheka kuelekea beach ya Kichangani uliokotwa mwili wa Mtu mmoja Mwanaume akiwa ameshafariki na baadaye mwili huo ulitambuliwa kuwa ni Abdallah Twahir Selemani Mkazi wa Chanika, awali Jeshi la Polisi lilipokea taarifa ya kupotea kwa Abdallah Twahir Selemani kutoka kwa Mama yake kuwa alipotea katika mazingira ya kutatanisha”
“Uchunguzi wa Jeshi la Polisi baadaye uligundua kuwa April 30, 2024 Mtuhumiwa Mussa Khamis Bakari (Buda) alikuwa na Marehemu wakitumia gari namba T.928 DFY Suzuki Kei wakitokea Magomeni kuelekea Temeke, Kijichi mpaka eneo ulipokutwa mwili wa Marehemu, uchunguzi wa vitu mbalimbali umebainisha Mtuhumiwa alimuua na baadaye kwenda kutupa mwili huo pembezoni mwa barabara ulipookotwa”
“Baada ya kumuua Mtuhumiwa alichukua kadi ya benki ya Marehemu na kwa nyakati tofautitofauti alianza kutoa pesa kiasi cha Tsh. milioni 61 kutoka kwenye akaunti ya Marehemu, chanzo cha mauaji ni tamaa ya kutaka kuiba pesa kutoka kwa Rafiki yake
ambaye sasa ni Marehemu, Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo”