Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila ameagiza kuondolewa majina 891 ya wafanyabiashara yaliyowekwa kwenye mtandao wa shirika la Masoko Kariakoo mpaka pale vyombo vya dola vitakapojiridhisha na majina hayo.
Hatua hiyo inakuja baada ya wafanyabiashara zaidi ya 800 waliokuwepo sokoni hapo kabla ya soko kuungua Julai 2021 kuandamana jana Alhamis, Julai 11,2024 kwenda ofisi za CCM Lumumba kupinga kutorejeshwa.
Katika orodha hiyo, wafanyabiashara 891 kati ya 1861 ndio walioelezwa kuwa na vigezo vya kurejea. Uamuzi huo uliwafanya kujitokeza katika viwanja vya mnazi mmoja kuhakikiwa na baada ya kutoridhishwa ndipo wakaandamana.
Chalamila ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Julai 12,2024 alipozungumza na uongozi wa shirika la Masoko Kariakoo katika ofisi ya Shirika la Masoko Magogoni.
Aidha Chalamila ameagiza Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza malalamiko ya wafanyabiashara kuwa majiana hayo yamewekwa kwa njia za rushwa huku akiwataka viongozi wa shirika la Masoko kujitafakari.