Klabu ya Chelsea imeingia kwenye sintofahamu baada ya kiungo Enzo Fernandez kuonekana akiimba wimbo unaodaiwa kuwa wa kibaguzi akiwa na wachezaji wenzake wa Argentina baada ya kushinda Copa America hali iliyopelekea ghadhabu miongoni mwa wachezaji na wapenzi wa soka huku mchezaji wa Chelsea, Wesley Fofana akiutaja wimbo huo kama “ubaguzi wa rangi usiozuiliwa”.
Wimbo huo ambao chimbuko lake ni ushindi wa Argentina wa Kombe la Dunia 2022 umewalenga wachezaji wa Ufaransa ambao wengi wao wana asili ya Afrika ukisema:- “Sikiliza, sambaza habari, wanacheza Ufaransa, lakini wote wanatoka Angola, wanaenda kukimbia. Kweli, wanapenda kulala na watu wa ‘trans’, mama zao ni Wanigeria, baba zao ni Wacameroon”
Kufuatia hatua hiyo kiungo Enzo Fernandez ameomba msamaha kwa kitendo chake katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii huku akibainisha kuwa alizidiwa na shangwe za sherehe za ubingwa wa Copa America 2024 na kusisitiza maneno hayo hayaonyeshi tabia au imani yake”.
Wakati huo huo Chelsea imelaani video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha kiungo wao huyo akiimba wimbo huo wa kibaguzi kuhusu wachezaji wa Ufaransa wenye asili ya Kiafrika huku wakithibitisha kuwa wamefungua hatua za kinidhamu dhidi ya nyota huyo.
“Klabu ya Soka ya Chelsea inaona aina zote za tabia za ubaguzi hazikubaliki kabisa. Tunajivunia kuwa klabu tofauti, jumuishi ambapo watu kutoka tamaduni zote, jamii na utambulisho wanajisikia kukaribishwa. Tunakubali na kuthamini msamaha wa mchezaji wetu hadharani na itatumia hii kama fursa ya kuelimisha Klabu imeanzisha utaratibu wa ndani wa nidhamu” imesema taarifa ya Chelsea.
Aidha Shirikisho la soka nchini Ufaransa (FFF) limeahidi kuwasilisha malalamiko FIFA kuhusu matamshi hayo ya kibaguzi ya wachezaji wa Argentina ambapo limesema: “Kwa kuzingatia uzito wa matamshi hayo ya kushtua ambayo ni kinyume na maadili ya michezo na haki za binadamu, Rais wa FFF ameamua kuwasiliana na mwenzake wa Argentina na FIFA moja kwa moja kuwasilisha malalamiko ya kisheria kwa matamshi ya kibaguzi na kibaguzi,”