Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Petro Magoti ametangaza dau la Tsh. elfu 50 kwa kila Mtu atakayempa taarifa ya sehemu ambako Wanafunzi wanachezeshwa unyago Wilayani humo akisema lengo ni kuhakikisha anakomesha kabisa unyago Kisarawe kwakuwa Watoto wanafundishwa vitu visivyo na maadili na vinavyozidi umri wao ikiwemo mafunzo ya kujiandaa kuwa na Wanaume yanayofanana na kitchen party.
Akiongea leo July 18,2024, Wilayani Kisarawe Magoti amesema “Nimesema hakuna kuchezesha Watoto unyago Wanafunzi, wakasema ‘ooh Magoti amezuia unyago unajua mambo ya Wazaramo!’ Wazaramo wa wapi?, Wazaramo na elimu?, kacheze wewe na Mkeo Mtoto wetu huyu anasomeshwa na Serikali hakuna unyago kwa Mwanafunzi”
“Na nimeshatenga fedha ili kuwalipa
Wanaoleta taarifa nataka nikamate Familia mbili niwapige show waelewe kwamba Mimi sio mchezomchezo namaanisha kwasababu Rais hawezi kuwa analeta pesa halafu unampiga mimba Mwanafunzi, ndani ya mwaka mmoja Wanafunzi 818 wameacha Shule, sasa tuna Shule 120 baada ya mwaka mmoja mwingine tunaweza kukuta Wanafunzi milioni 2 hawaendi Shule”
“Nimeona Mama mmoja alinitumia ujumbe namuheshimu sana ananiambia ‘acha Watoto wacheze unyago wewe unawazuia Watoto ni wako?’ Mama namuheshimu sana yule sitaki nimtaje, niliandika mara ya kwanza nikafuta, ya pili nikafuta ya tatu nikasema nimfuate nikasema hapana, na Watoto wake nawajua hawajachezewa unyago”
“Unyago ni kitchen party tofauti ni kwamba kitchen party unajua Mume wangu ni huyu, unyago unamwandaa Mtoto aende akaolewe na Watoto wetu wengine wananengua kuliko Mama zetu Watu wanawapiga mimba, na nimesema nimepandisha dau sasa hivi ukiniletea taarifa ya unyago nakupa Tsh . elfu 50, nikifika penye unyago yule aliyeleta naondoka nae, Mashangazi ndio nimesikia wana nongwa nawachukua wote na yule aliyealikwa kutoka Mkoani namchukua na tumeanzisha kilimo cha ufugaji wa kuku, unafanya usafi kwenye shamba la Wajane mpaka unakonda macho, Mtu aliyesoma huwezi kumpeleka Mwanafunzi kucheza unyago”