Kope za mtu za asili hufanya kazi muhimu, hulinda macho dhidi ya vumbi na hata hewa kuzifikia mboni ya jicho, na humwezesha mtu kupepesa macho, hatua ambayo pia huhakikisha kwamba macho yana majimaji vizuri.
Kope bandia hushikanishwa na kope za asili, kwa kutumia gundi ambayo inaweza kusababisha matatizo.
Kemikali zilizoko kwenye gundi, mbali na kiweza kusababisha mzio (allergy) inaweza kuwasha eneo la jicho na uzito wa gundi yenyewe inaweza kusababisha mwasho kwenye kope.
Kumekuwa na ripoti za watu ambao kope zao zimeshikamana kwa sababu ya matumizi ya kope bandia.
Utafiti mmoja ulionesha kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wanawake waliripoti changamoto ya tatizo la keratoconjunctivitis, hali ya jicho inayohusisha kuvimba kwa kornea na kiwambo cha jicho kwa wakati mmoja, baada ya gundi ya kope bandia kugusa macho yao.
Utafiti huo uligundua kuwa asilimia 40 ya wanawake walipata athari ya mzio kutokana na gundi.
Kumekuwa na nyakati ambapo gundi ya kucha, ambayo ina nguvu zaidi imeuzwa kama gundi ya kope.
Katika mojawapo ya matukio ya kushtua sana ya utumiaji usiofaa wa gundi, kope za mwanamke ziliachwa zikiwa zimeshikamana pamoja baada ya kuweka kope bandia kwa kutumia gundi kali.
Gundi ya kope inaweza kusababisha hatari kadhaa za afya. Utafiti mwingine ulichanganua viambata 37 vya kibiashara na kitaalamu na kugundua uwepo wa kemikali ya formaldehyde inayojulikana kusababisha saratani.
Uchambuzi huo uligundua kuwa asilimia 75 ya viambata 20 vya kitaalamu vilivyojaribiwa vilitoa formaldehyde, na gundi nne kati ya 17 za kibiashara pia zilikuwa na kemikali hiyo hatari.