Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imebaini kuwa, madai ya Mbunge wa Babati (CCM), Pauline Gekul na wenzake kudaiwa kuwafanyia vitendo vya ukatili na udhalilishaji vijana wawili waliokuwa wafanyakazi wake, hayakuweza kuthibitishwa.
Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Julai 19, 2024 jijini Dodoma na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na utawala bora kwa mwaka 2022/23.
Amesema tume hiyo ilifanya uchunguzi wa tuhuma hizo zinazodaiwa kufanywa na Gekul aliyedaiwa kutenda kosa hilo Desemba 2023 kwa Hashim Philemon na Michael Marishamu kwa kuwaingizia chupa sehemu ya haja kubwa ili waseme ukweli, kuhusu kumwekea sumu kwenye chakula na kuweka vitu vya uchawi kwenye hoteli yake ya Paleii Lake View.
Mwenyekiti huyo amesema baada ya uchunguzi, tume kwa kuzingatia maelezo ya watu mbalimbali waliohojiwa na vielelezo ambavyo tume imevipitia haikubaini suala hilo kufanyika.
“Hata hivyo tume ilibaini walalamikaji walizuiliwa kwa muda mrefu wakati wakihojiwa na mlalamikiwa kuhusu tuhuma za kutaka kumwekea sumu (Pauline Gekul) pamoja na kupeleka madawa ya kishirikina katika hoteli yake na hivyo kusababisha walalamikaji kukosa haki yao ya kuwa huru,” amesema Jaji Mwaimu.