Kwanini Kilichomfika Trump Ni Vigumu Kumfika Komredi Kim Jong Un..?
Jibu:
Dunia ingali na mshangao wa ilikuwaje Rais wa Taifa kubwa la Marekani apigwe risasi katika mazingira yaliyoruhusu kijana wa miaka 20 kuparamia paa la nyumba jirani na alikosimama Trump.
Duru za Kijasusi ulimwenguni zinaelekeza vidole vya shutuma kwa majasusi walinzi wa Trump.
Marekani ‘ Secret Service Agents’ kwa maana majasusi walinzi wa Rais wana jukumu moja kubwa; kuwalinda Marais, wakiwemo Marais wastaafu na kuwalinda viongozi.
Usiku ule wa Jumamosi tulioangalia moja kwa moja tukamwona Trump akianza kuongea na ghafla milio ile ya risasi ikasikika. Tukamwona Trump akijiangusha chini akisaidiwa na walinzi wa nyuma yake.
Mara tukawaona majasusi wale walinzi wa Rais wakikimbia kwa kasi kuelekea jukwaani kutoka pande mbili, kushoto na kulia. Ni jamaa wale wenye kuvaa makoti myeusi na miwani myeusi.
Mara walinzi wale wakasimama na Trump anayechuruzika damu. Trump yule akahakikisha ananyanyua mkono akikunja ngumi huku akitamka;
“ Fight .. fight..!”
Trump kama alivyosema mwenyewe baadae, kuwa aliiona fursa kwenye janga lile kwamba Wamarekani na dunia nzima ingeangalia alichokifanya na kusikiliza alichokisema.
Lakini, tunarudi kule kule, je, Secret Service Agents wa Marekani kwanini mpaka mwaka huu wa 2024 wameshindwa kuzuia kilichowatokea marais 15 wa Marekani kuanzia Abraham Lincoln aliyeuawa mwaka 1965 mpaka Ronald Reagan aliyenusurika kuuawa mwaka 1981?
Kumbukumbu ni kuwa Marais 15 wa Marekani kwenye historia, wamekumbwa na kadhia ya kushambuliwa kwa risasi. Kati yao watano walipoteza maisha.
Swali:
Kwanini kilichomtokea Trump ni vigumu kumtokea Komredi Kim Jong Un wa Korea Kaskazini?
Jibu:
Kwa Kim kupigwa risasi itakuwa ni sawa na ngamia kupenya kwenye tundu ya sindano.
Jamaa yule maarufu kwa staili yake ya kunyoa kiduku, yuko vizuri sana kwenye eneo la majasusi ‘ Makomandoo’ walinzi wa Rais.
Kuna mizunguko kama saba hivi ya majasusi walinzi wa Rais Kim. Kwenye wa mzunguko wa saba huko ndiko labda unaweza kuwakuta ‘ wenye kuuza madafu!’
Wote wenye silaha jirani na Kim ni walinzi wake tu.
Kim hali wala hanywi chochote ambacho hakijapimwa na kuonjwa na mwingine kabla yake.
Akisafiri kwa treni ni kwenye treni maalum ambayo haipenyi risasi. Nje ya nchi anasafiri na choo chake. Hofu ni kuwa kwenye vyoo vya ugenini adui anaweza kukusanya haja za Rais ili kupima DNA ya Kim.
Je, Majasusi ‘ Makomandoo’ wake wanapatikanaje?
Jibu:
Hawa ni watu maalum kabisa waliopata mafunzo maalum. Sifa nne za kuwa kwenye kikosi cha majasusi walinzi wa Komredi Kim Jong Un moja ni kuwa hodari kwenye mchezo wa Taekwondo.
Watu wenye mafunzo ya Taekwondo wana uwezo wa kupambana hata kwa kurusha visu au kutumia mikono na miguu. Wana uwezo pia wa kupambana wakiwa wanaogelea majini.
Sifa ya pili ni UTIIFU kwa Kim Jong Un, na ndiyo sifa ya tatu na nne, UTIIFU kwa Komredi Kim Jong Un.
Ni majasusi hawa walinzi wa Komredi Kim Jong Un utawaona wakisindikiza Limousine iliyombeba Kim wakiwa kwenye kukimbia tu. Ni kwa umbali mrefu.
Vimo vyao kwa maana ya urefu havipaswi kuwa zaidi ya urefu wa ‘ Bosi’ wao, Kim Jong Un.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.