Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limemkamata Dada wa kazi za nyumbani (House Girl), Clemensia Cosmas Mirembe (19) aliyekuwa anatafutwa kwa kosa la kumjeruhi Mtoto wa Boss wake Maliki Hashimu (5) Mkazi wa Goba Jijini Dar es salaam ikidaiwa alimkata na kitu chenye ncha kali shingoni kilichotenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kumsababishia kushindwa kupumua, kuongea, kupata maumivu na kupoteza damu nyingi sana.
Akiongea leo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Jumanne Muliro amesema ——— > “Baada ya tukio Mtuhumiwa alikimbia, upelelezi wa tukio hilo la kikatili ulianza mara moja na July 21, 2024 saa 4:00 usiku Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumkamata Mtuhumiwa huyo akiwa amejificha kwenye jumba bovu maeneo ya Goba Kizudi Kinondoni”
“Mtuhumiwa huyo anahojiwa kwa kina na atafikishwa Mahakamani haraka iwezekanavyo kwa hatua zaidi za kisheria, nitoe wito na kuwawashauri Wazazi, Walezi, Walimu na Jamii kwa ujumla kuwafundisha Watoto kujenga tabia ya kutembea katika makundi lakini pia Watoto wasikubali kuwa karibu na Watu wasiowafahamu, Watoto wasitumwe maeneo ambayo kwa mazingira ni hatarishi ikiwa ni pamoja na kuacha kuwatuma Watoto wadogo maeneo mbalimbali nyakati za usiku”
Mtoto huyo alijeruhiwa Julai 15,2024 majira ya saa 12 jioni eneo la Goba Kinzudi, Kinondoni ambapo alipelekwa Hospitali ya Mloganzila na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anapoendelea kupatiwa matibabu mpaka sasa, Polisi iliahidi kuwa Mtuhumiwa lazima akamatwe na leo imetangaza kufanikisha hilo.