Nape Nnauye Ameponzwa na Mdomo au Utendaji Wake wa Kazi?

0:00

11 / 100

MAKALA

Usiku wa kuamkia leo Jumatatu tumefikiwa na taarifa za kutoka Ikulu, kuwa mmoja wa Mawaziri na wanasiasa nguli, Nape Nnauye, ni mmoja wa aliyeondolewa kwenye Baraza kufuatia ‘ Teuzi na Tenguzi’ za Rais wa Jamhuri.

Siku ile niliposikiliza clip ya Nape akiwa Bukoba nikaanza kutafakari hatma yake. Kimsingi niliziona siku za Nape kwenye Uwaziri zinazohesabika.

Katika Sayansi ya Siasa, Nape angepata huruma za wananchi kama, mara baada ya kung’amua kosa alilofanya, angejishusha chini na kuomba msamaha bila kuingiza maneno kama “ Ilikuwa utani”. Suala la uchaguzi na kura linahusu maisha ya watu. Si la kufanyia utani.

Matokeo yakawa tulivyoyaona, Waziri wa Mitandao kimsingi ameangushwa na watu wa mitandaoni pia. Ni kwa kauli zake.

Na Rais wa Jamhuri, Dr. Samia Suluhu Hassan ameonyesha weledi mkubwa. Ni kwa kuacha umma ukiwemo wa mitandaoni, umsomee Nape ‘ mashtaka’ yake na hivyo kumrahisishia Rais wa Jamhuri kupitisha hukumu yake.

Imetoa tafsiri pia, kuwa Ofisi ya Rais chini ya Rais ina wenye kuifanya kazi yao. Na kwamba wana kazi inayoendelea.

Shamsi Vuai Nahodha alipata kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mwaka 2013, Kiongozi huyu, Shamsi Nahodha, alipata kutoa kauli yenye hekima na busara nyingi. Ni juu ya umuhimu wa viongozi kuchunga kauli zao.

Nahodha alialikwa kwenye kusanyiko la viongozi wa kidini lilioandaliwa na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kujadili juu ya hali iliyojitokeza wakati huo kwenye jamii yetu. Hali ya misuguano ya kidini.

Waziri Nahodha alisema, kuwa yanayotamkwa na viongozi hayaishii pale yanaposemwa tu. Hutafsiriwa kwa maana iliyokusudiwa, au hata ile ambayo haikukusudiwa. Hivyo, umuhimu wa kuchunga kauli .

Na hakika, hapa duniani kuna mifano ya viongozi, ambao kupitia kauli zao, ama, zimewajenga, au zimewabomoa kisiasa.

Na siku zote, historia ni mwalimu mzuri. Nimepata kukumbushia hilo mara nyingi. Maana, ili tuweze kutafsiri na kuyaelewa yanayotokea sasa, na kuyaelewa yatakayotokea kesho, tuna lazima ya kuangalia na kutafsiri kilichotokea jana. Na hii ni moja ya maana ya kusoma na kutafsiri alama za nyakati.

See also  JINSI SERIKALI YA TANZANIA INAVYOTUMIA MABILIONI KWAAJILI YA TIMU ZA TAIFA

Katika hili la kauli, hapa kwetu Tanzania kuna kisa cha Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa mwaka 1985. Mzee John Malecela alikuwa bado na ujana wa kisiasa. John Malecela, katika uchaguzi ule wa mwaka 1985, ndiye alikuwa waziri pekee katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa na ambaye hakurudi bungeni. John Malecela alikataliwa na wapiga kura wake. Hakurudi bungeni.

Kwanini?

Kwa mujibu wa maandiko ya wasomi watafiti, marehemu Bw. Mvungi na Bw. Amos Mhina ( Searching for a people MP?), anguko la John Malecela lilitokana na kukosa uzoefu na mahusiano mazuri na wapiga kura katika ngazi za chini.

Huyu alikuwa John Malecela ambaye ndugu yake Job Lusinde ndiye alikuwa mbunge aliyemtangulia jimbo la Dodoma Mjini. Malecela alibwagwa na injinia asiye na uzoefu wa kisiasa, aliitwa Mazengo Yohana.

Hata hivyo, katika hili la mahusiano na watu, watafiti wale katika maandiko yao kwenye kitabu kiitwacho, “Tanzania, Democracy In Transition”, kwa mtazamo wangu, wameshindwa kubainisha sababu nyingine iliyochangia kuharakisha anguko la John Malecela wa wakati huo. Hili linahusiana pia na mahusiano kati ya John Malecela wa wakati huo na wapiga kura wake na hata Watanzania kwa ujumla.

Kati ya sifa za Watanzania zilizojengeka na kurithishwa kwenye vizazi, ni kutopenda kupuuzwa, kubezwa, kudharauliwa na kunyanyaswa. Na yeyote yule.

Na kama matendo hayo yatafanywa na viongozi wao, Watanzania, pamoja na kuonekana wapole machoni, wana uwezo wa kutoa adhabu kali sana na isiyo na huruma.

Na hapa tuangalie kauli ya John Malecela wakati huo akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.

Katikati ya kilio cha Watanzania watumiaji wa njia ya reli ya kati (TRC) juu ya huduma mbaya za Shirika hilo la Reli miaka ile ya 80, Bw, John Malecela, akiwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, alipata kukaririwa akitamka, kuwa hakukuwa na tatizo la huduma mbaya, na kwamba, wenye kufikiri hivyo, alitamka;

See also  Spanish police arrest three over racist insults at El Clasico match

“ They can go to hell!”

Kwamba wanaweza kwenda kuzimu. Na kwa hakika, mzimu wa kauli yake ile kwa Watanzania Wanyonge, uliendelea kumwandama Malecela na hata, kwa mtazamo wa sisi wachambuzi, ulimgharimu kupata tiketi ya kugombea urais kupitia CCM.

Katika sanaa ya mawasiliano, tunaamini, kuwa sentesi moja inayotamkwa na mwanasiasa, yaweza kumjenga au kumbomoa kabisa kisiasa mwanasiasa husika.

Kwa John Malecela, kauli yake ile ataishi asiisahau, maana, pamoja na kuwa tulikuwa katika mfumo wa chama kimoja, redio moja ya taifa na magazeti matatu, bado wananchi waliweza kufikisha shutuma zao kwa Malecela juu ya kauli yake ile.

Utotoni nikiwa Shule ya Msingi, nakumbuka kusoma barua nyingi kwa Mhariri, za Wasomaji wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo wakimlaani Malecela.

Na kilichotokea katika uchaguzi mkuu uliofuata wa mwaka 1985, ilikuwa ni kwa wapiga kura wa Dodoma Mjini kushindilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la kisiasa la John Malecela.

Walifanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wengine na hususan watumiaji wa reli ya kati. Malecela aliangushwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Hakupata ubunge na hivyo hakuweza kuwa Waziri.

Na hakika, Malecela alijifunza, na hata aliporudi tena kwenye ulingo wa kisiasa, Mzee John Malecela, hata hii leo, amekuwa ni makini sana katika kuchagua maneno anapowasiliana na umma. Ukimsikiliza Malecela wa leo, wala usije ukadhani ana kigugumizi, Mzee Malecela ni fundi wa kuchagua maneno. Anafikiri kisha anaongea, haongei halafu ndio afikiri.

“Nahofia, kwa hali tunayokwenda nayo sasa, kuwa yaliyomkuta Mzee wetu John Malecela miaka zaidi ya 20 iliyopita, huenda yatakuja kuwafika baadhi ya wanasiasa wetu wa sasa, na wengine ni mawaziri wenye dhamana. “

See also  Before venturing into poultry agribusiness, consider the following steps.

Niliyaandika hayo kupitia Raia Mwema Mei 13, 2013.

Kwamba ya enzi za akina Malecela yatakuja pia kuwafika baadhi ya wabunge, ambao, wakiwa bungeni na nje ya bunge, kwa kauli zao zisizo makini, wanajisahau, kuwa kuna wengi wenye kuwasikiliza.

Kwanini?

Wapiga kura wa leo ni wenye uelewa zaidi kuliko wale wa 1985. Wapiga kura wa leo sio tu wanakumbuka na kufuatilia matendo ya wabunge wao na hususan ahadi walizotoa ambazo hazikutimizwa, bali, wanakumbuka, na wataendelea kuzikumbuka pia, baadhi ya kauli za kejeli kwa wapiga kura kutoka kwa baadhi ya wabunge na mawaziri.

Na mara nyingi kuna kosa kubwa linalofanywa na wanaotafiti hali ya kisiasa. Wengi wa watafiti wanalenga zaidi katika kuchambua mienendo ya wagombea na kampeni zao.

Watafiti hawa wamesahau kutafiti mienendo ya wapiga kura ambao kimsingi ndio wenye uchaguzi na maamuzi ya nani awe kiongozi wao.
Na moja ya hulka za mpiga kura ni kujaribu kukumbuka kauli za nyuma za wagombea.

Hivyo, wito kwa wanasiasa wa leo, na wengi wao ni vijana, kuwa wasome historia, wasome vitabu na watafute uzoefu kwa kuwasikiliza waliotangulia.

Wairejee pia kauli ya hekima ya Waziri Vuai Shamsi Nahodha, kuwa kuna umuhimu wa viongozi kuwa makini kwenye kauli zao.

Loading

Mujuni Henry
Author: Mujuni Henry

JUNIITV

Related Posts 📫

Brighton's Welbeck completes comeback win over Tottenham
Tottenham Hotspur's second-half capitulation to lose 3-2 at Brighton and...
Read more
Schmidt giving wounded Wallabies emotion on his...
Dublin was always going to be rugby party central this...
Read more
Nchini Korea Kaskazini kama "Birthday" yako ni...
Sababu kubwa ni kwamba tarehe hizo Baba wa Taifa hilo...
Read more
Mwili wa Ebrahim Raisi wapatikana
BREAKING NEWS Mwili wa aliyekuwa Rais wa Iran, Ebrahim Raisi...
Read more
HOW TO SATISFY YOUR MAN
Learn it, practice it. Look deep into his eyes and make...
Read more

Leave a Reply