Nyota mpya wa klabu ya Yanga Sc, Chadrack Boka bado hana uhalali wa kuwatumikia waajiri wake hao wapya baada ya klabu ya FC Lupopo kushindwa kuipatia Yanga Sc Cheti cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) huku ikibainika kuwa FC Lupopo sio mmiliki halali wa nyota huyo raia wa DR Congo.
Klabu ya AC Real de Kinshasa imewasilisha barua ya malalamiko kwenda Shirikisho la soka DR Congo ikidai Boka ni mchezaji wao halali na alikwenda kwa mkopo FC Lupopo kwa msimu wa 2022/23.
Barua hiyo ya malalamiko imeeleza kuwa FC Lupopo ilikutana tena na AC Real de Kinshasa kujadili upya mkataba wa mkopo wa misimu miwili ya 2023/24 na 2024/25 kwa makubaliano ya dola 15000 kwa msimu.
Hata hivyo FC Lupopo ililipa dola 15000 tu ya mkopo wa msimu wa 2023/24 huku ikishindwa kurejea kwa ajili ya malipo ya dola 15000 zingine kwa msimu wa 2024/25 hivyo bado wanadaiwa na bado imempiga bei nyota huyo kwenda Yanga Sc.
Aidha moja ya masharti ya makubaliano hayo ya mkopo ni kwamba ikiwa mchezaji huyo atatakiwa na timu nyingine basi Real de Kinshasa itanufaika na 70% za mauzo huku FC Lupopo ikinufaika na 30%.
Kulingana na maelezo hayo klabu ya Yanga Sc imenunua mchezaji ambaye alikuwa kwa mkopo FC Lupopo hivyo Wananchi watatakiwa kuwasiliana na kujadiliana upya na AC Real de Kinshasa ili kuipata ITC.