Serikali ya Tanzania imekubali kuilipa kampuni ya Australia, Indiana Resources Limited fidia ya Dola milioni 90 za Marekani (sawa na Sh237 bilioni), baada ya kuafikiana kutokana na kusitishwa leseni ya mradi wa Ntaka Hill Nickel wa madini ya sulfidi ya nikeli ulioko mkoani Lindi.
Katika taarifa iliyotolewa Julai 29, 2024 na kampuni hiyo imeeleza kuwa uamuzi huo ulitolewa Julai 26, 2023 na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) ambapo awali uliitaka Tanzania kulipa fidia ya Dola milioni 109 za Marekani (zaidi ya Sh 286 bilioni za kitanzania), baada ya kujiridhisha uwepo wa ukiukwaji wa mkataba wa uwekezaji katika mradi wa Nikeli wa Ntaka Hill mwaka 2018.
Aidha tayari Tanzania imeshalipa dola milioni 35 (sawa na shilingi bilioni 92) kisha watalipa Dola millioni 25 (sawa na shilingi bilioni 65) kabla ya Oktoba 25, 2024 huku kiasi kilichobaki cha dola milioni 30 (sawa na Shilingi bilioni 78) kikitarajiwa kulipwa kabla au siku ya tarehe 30 Machi 2025.
“Tanzania itahitajika kukamilisha kiasi kilichobaki katika awamu mbili, Dola milioni 25 ifikapo Oktoba 25, 2024 na Dola milioni 30 ifikapo Machi 30, 2025″ Imeeleza taarifa hiyo.
Mgogoro kati ya Indiana Resources na Tanzania ulitokana na mabadiliko ya Sheria za Madini za Tanzania mwaka 2017 na 2018. Januari 10, 2018, kupitia kanuni zake za Haki za Madini za 2018, Tanzania ilitangaza kuwa leseni zote za uhifadhi zilizotolewa kabla ya tarehe ya kuchapishwa kwa kanuni hizo zilifutwa na zitakoma kuwa na athari za kisheria.