Ujasusi Wa Israel Ndani Ya Ardhi Ya Iran…
Ismael Haniyah anazikwa Qatar leo Ijumaa. Mauaji yake ndani ya Teheran ni kazi ya Mossad, Shirika la Ujasusi la Israel.
Swali:
Ilikuwaje Mossad wafanye mauaji ndani ya ardhi ya Iran?
Jibu:
“ Adui wa mbali anapokuja kwenu, kuna wenyeji wenye kumpa maji ya kunywa anaposhikwa na kiu.”- John Malecela.
Mzee Malecela alipata kuyasema hayo pale Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam ulipolipuliwa na magaidi miaka ya 1990.
Mzee Malecela alikuwa sahihi. Miaka kadhaa iliyofuata, ikagundulika, kuwa kuna Mtanzania aliyehusika na tukio lile na kwamba alikuwa kwenye mtandao wa Alqaida ya Osama Bin Laden.
Tukirudi kwa kilimchotokea Ismael Haniyah, Israel kupitia Mossad, waliwahi kumfanyia Mohsen Fakhrizadeh, Mtaalam bingwa wa masuala ya nyuklia wa Iran.
Mohsen Fakhrizadeh aliuawa na Mossad, ndani ya Jiji la Teheran, Iran. Ilikuwa Novemba 27, 2020.
Hivyo, Mossad wamefanya hivyo kabla, na si kwa mtu mmoja.
Swali:
Wanafanyaje Mossad?
Jibu:
Operesheni za kijasusi za Mossad huwa si za kitoto. Maandalizi ya operesheni moja kubwa hadi kutekelezwa kwake huchukua kuanzia nusu mwaka hata mwaka mzima.
Tuchukue mfano wa Mohsen Fakhrizadeh. Walijua njia anayopita kwa gari lake anapotoka nyumbani. Mossad kuna mahali kwenye njia hiyo waligundua kuna gari mkweche, ama gari bovu.
Gari hilo lilikuwa limetelekezwa tu kando ya njia. Mossad ndani ya Iran wana mawakala wao wa kulipwa. Kuna waliyempa kazi kwenye hilo la gari mkweche.
Mossad wakaanza kuingiza silaha kwa vipande vipande. Silaha hiyo ikawa inaunganishwa taratibu ndani ya gari lile mkweche. Hata ikakamilika.
Hatua iliyofuata ikawa kuiunganisha silaha hiyo na kwenye mfumo wa ‘ Akili Mnemba’- Artificial Intelligence. Ni mfano ule wa ‘ Robot Yunus’!
Basi, ‘ Robot Yunus’ wa Mosssad mwenye silaha, ndani ya gari mkweche, Teheran, Iran, akawa anaongozwa na majasusi wa Mossad wakiwa Tel Aviv, Israel.
Na ikafika siku ya tukio, Novemba 27, 2020. Wakati gari la Mohsen Fakhrzadeh likipita kando ya gari mkweche, risasi zikaunguruma na kummaliza Mohsen Fakhrizadeh.
Ili kufuta nyayo. Majasusi wale wa Mossad walio Tel Aviv, Israel, wakalilipua pia gari lile mkweche.
Hivyo, wakamlipua pia, robot wao ‘ Yunus”.