Madiwani,wenyeviti wa vijiji na baadhi ya wakazi wa tarafa ya Ngorongoro wametoa tamko la kusikitishwa na kitendo cha tarafa hiyo kutotajwa kama sehemu ya vituo vya uboresha daftari la mpiga kura.
Diwani wa Kata ya Alaitolei James Moringe amesema baada ya kufuatilia amebaini jina lake na majina mengine yamehamishwa na kutakiwa kushiriki uchaguzi kupitia vituo vya kupigia kura vilivyoko Msomera mkoani tanga.
Moringe amesema wameshangazwa na kitendo hicho kwakuwa kinawanyima haki ya kupiga kura wakazi zaidi ya laki moja na elfu tatu ambao wameamua kubaki na kuishi katika tarafa hiyo.
“Ni jambo ambalo limekuja kutukumbusha majeraha ambayo wakati mmoja tulisemekana sisi ni Wasudan,tumetoka Sudan ,haya imetoka hiyo leo sasa tunaambiwa hatuwezi kupiga kura,unaenda kuniadika katika eneo ambalo sijahamia” amesema Moringe.
Naye Shutuk Kitamwasi diwani kata ya Alailelai amesema wamevumulia mengi yaliyowaumiza na kuwa ni wakati sasa watachukua hatua zikiwemo za kisheria dhidi ya vitendo hivyo kikiwemo kitendo cha kunyimwa haki ya kupiga kura.
“Ninasikitika sana kusikia kuna tume huru ya uchaguzi wakati kitendo walichokifanya Ngorongoro kinawanyima sifa ya kuwa Tume huru,waendelee tu kuiita Tume ya Uchaguzi,kwa sababu sio tume huru,huo uhuru uko wapi?” amehoji Kitamwasi
Hivi karibuni kumetolewa orodha ya vituo vitakavyotumika kuboresha daftari la mpiga kura katika maeneo mbalimbali nchini huku Tarafa hiyo hiyo ikiwa haimo katika orodha hiyo jambo lililozua gumzo kwa wakazi wa tarafa hiyo.