Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata na linamuhoji kwa kina Amos Lutakulemberwa Lwiza mwenye umri wa miaka 54 mkazi wa Tegeta Wazo Kinondoni kwa tuhuma za kusambaza taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuwa binti anayedaiwa kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji amekutwa amefariki jambo ambalo ni uongo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Agosti 7, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam SACP Muliro Jumanne Muliro amesema kuwa watu wajiepushe kusambaza taarifa za uongo kwani zimekua zikizusha taharuki ndani ya jamii.
“Jeshi la Polisi linatoa wito watu kujiepusha na kutoa au kuchapisha taarifa za uongo zenye malengo ya kuzusha taharuki katika jamii kwani kufanya hivyo ni makosa lakini litaendelea kuzingatia maoni ya watu ambayo hayakinzani na sheria za nchi”amesema SACP Muliro.
Akizungumzia kuhusu hali ya usalama kuelekea mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Simba katika Uwanja wa Benjamini Mkapa SACP Muliro ameeleza kuwa Jeshi hilo limechukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo.
“Usalama utaimarishwa kwa kiwango cha juu,hivyo tunawakumbusha nimarufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo, watu watakaojihusisha na vitendo vyakihalifu ndani au nje ya uwanjawatashughulikiwa haraka kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza SACP Muliro.
Mchezo wa soka wa watani wa jadi baina ya klabu ya Yanga na Simba zote za Dar es salaam utachezwa kesho kuanzia saa 1:00 jioni Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.