Kesi inayowakabili washtakiwa tisa wanaodaiwa kumuua Asimwe Novath, mtoto aliyekuwa na ualbino na kisha kukata baadhi ya viungo vya mwili wake wilayani Muleba Mkoani Kagera, imehamishiwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Bukoba kutoka mahakama ya hakimu mkazi Bukoba ilikokuwa kwa ajili ya hatua za awali.
Washtakiwa hao tisa wamesomewa maelezo ya awali na Wakili wa Serekali, Erick Mabagala juu ya kuhusishwa kwao na shtaka linalowakabili la mauaji ya kukusudia ya Asimwe, Mei 30 mwaka huu.
Wakili amesema upande wa mashtaka unatarajia kuleta mashahidi 52, vielelezo 37 huku upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mathias Rweyemamu ukiandikisha mashahidi 20 pamoja na vilelezo kadhaa ikwemo simu za mkononi.
Mahakama hiyo pia imepokea ombi la mshtakiwa namba saba, Faswiru Athumani la kuwapatia mawakili washtakiwa ambao hawana mawakili wa kuwatetea katika shauri hilo.
Upande wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya mtoto mwenye ualbino, Asimwe Novath (2) umewasilisna maelezo ya ushahidi katika hatua ya awali, ukieleza utakuwa na mashahidi 52 na vielelezo 37.
Katika maelezo hayo ya ushahidi mmoja wa mashahidi ameeleza mbinu iliyotumiwa na washtakiwa kumpora mtoto huyo na kutokomea, pia ikitajwa ahadi ya gari aina ya Toyota Landcruiser V8, maarufu kama “Shangingi” kwa baba wa mtoto.
Asimwe aliporwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwao kijiji cha Bulamula, Kata ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera, Mei 30, 2024 saa 2:00 usiku na kutokomea kusikojulikana.
Siku 17 baadaye mabaki ya mwili wake yalipatikana yakiwa yamefungwa kwenye mfuko wa sandarusi na kutelekezwa chini ya kalavati lililoko barabara ya ya Makongora, Kitongoji cha Kabyonda, Kata ya Ruhanga wilayani humo.
Siku kadhaa baadaye, Jeshi la polisi lilitoa taarifa ya kuwashikilia watu tisa akiwemo baba wa marehemu, Novath Venanth na Padre Elpidius Rwegoshora na kuwafungulia kesi ya mauaji namba 1774/2024, katika mahakama ya wilaya ya Bukoba mkoani humo.