Mbunge wa Keiyo Kusini, nchini Kenya, Gideon Kimaiyo, aliapa kwamba hatooa hadi atakapopata shahada ya uzamivu (PhD), sasa amefanikiwa kuipata na yuko tayari kuoa.
Mbunge huyo amesema alijiwekea ahadi hiyo akiwa kijana huku akisoma kwa shida kutokana na umaskini wa familia yake.
Jana Septemba 20, 2024, mbunge huyo mwenye umri wa miaka 37 alitimiza ndoto yake kwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Masuala ya Mahusiano ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
“Ndio, nimetimiza ndoto yangu na sasa niko huru kuoa hata kama ni sasa baada ya kumaliza sherehe ya kuhitimu,” alijibu kwa utani jana wakati wa sherehe ya wanandugu kumpongeza huku akicheka.
“Nilipoingia kwenye siasa, watu walisema nisingechaguliwa kwa sababu sikuwa na mke, watu wangeniona mhuni. Walinishauri kwamba ninapaswa kumtafuta mwanamke na kufunga naye ndoa haraka haraka. Nikasema ‘Hapana’.”
Ili kuthibitisha jinsi alivyo na msimamo thabiti, anasema hakutahiriwa hadi alipomaliza sekondari. Anasema aliamua kuchelewesha tohara kwa sababu hakutaka kufuata njia ya kawaida kama wavulana wenzake katika eneo lake.
Anasema wavulana wenzake wengi baada ya tohara walikuwa wanageukia ndoa na wapo wenye watoto saba!
Akiwa mtoto wa sita kati ya watoto tisa, anasema anatoka kwenye familia maskini iliyokuwa ikiuza pombe, na kulikuwa na siku ambazo aliporudi nyumbani na kukuta watu wakifurahia pombe lakini hakuna chakula.