Taarifa za kuuawa kwa Katibu Mkuu wa Chama cha siasa Hezbollah cha Lebanoni, Sheikh Sayyed Hassan Nasrallah zimeitikisa dunia baada ya Jeshi la Israeli kutangaza kumuua na Hezbollah kuthibitisha taarifa hizo. Lakini kwa hapa Tanzania taarifa hizo zimepokelewa kwa hisia tofauti huku watu wengine wakiuhusisha mgogoro wa Lebanoni na Israeli kuwa wa kidini unaohusisha dini za Kikristo na Kiislamu.
Mara nyingi, imeandikwa na kutanabaisha kuwa mgogoro wa Mashariki ya Kati unaohusu Israeli na Lebanon, Israeli na Jordan, Israeli na Palestina, Israeli na Syria au hata Israeli na Misri sio wa kidini bali ni mzozo wa koo, jamii, madaraka nk. Katika andiko hili, Askofu atatoa ushahidi kuonesha kuwa mzozo huo sio wa kidini.
Hezbollah ni Chama cha Siasa nchini Lebanon kilicho na wingi wa viti vya Bunge ambapo idadi yake ni 12% katika Bunge lote la Lebanon. Chama hicho kina mlengo wa Uislamu wenye siasa kali na wanachama wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia wanaoungwa mkono sana na nchi ya Iran.
Asilimia 95 ya wananchi wa Lebanoni ni jamii za Waarabu, asilimia 4 ni jamii za Waarmenia na asilimia 1 tu ndio jamii nyingine. Kwa hiyo, kwa ujumla Lebanoni ni nchi ya Kiarabu.
Katiba ya Lebanoni inataka Rais wa Lebanoni ni lazima atoke katika Dini ya Kikristo na katika Kanisa la Maronite. Kanisa hili ndilo Kanisa kongwe kabisa Lebanoni. Ndio hilo linaloitwa Syriac Church ambalo lilianzishwa na Mtume Paulo pamoja na Mtume Barnaba miaka 20 au 25 baada ya kufa na kufufuka kwa Yesu (soma Matendo ya Mitume 13:1-52). Kanisa hili ndilo liliitwa Kanisa la Antiokia ambalo baadaye pia liliwahi kuongozwa na Askofu Mkuu Ignatius (Inyasi wa Antiokia).
Kanisa la Antiokia ni Jimbo la Pili kuanzishwa baada ya Jimbo la Yerusalemu ambapo pia lilianzishwa baada ya kupata uhuru kutoka Kanisa mama la Yerusalemu baada ya mzozo au mgogoro wa Mitume kuhusu kufuata au kutokufuata tamaduni za Kiyahudi (Matendo ya Mitume 15:1-35).
Baada ya mpasuko mkuu wa Kanisa Katholiko mwaka 1054 uliozaa Orthodox Catholic na Roman Catholic, Kanisa la Antiokia likabakia upande wa Orthodox Catholic Church maarufu kama Eastern Orthodox Church pamoja na Greek Orthodox na Russian Orthodox Church.
Kutokana na historia hiyo, Kanisa hili ndilo pia dini kongwe kuliko zote nchini Lebanoni na pia ndio limepewa hadhi ya kutoa Rais wa Jamhuri ya Lebanoni. Ukumbukwe kuwa Uislamu nchini Lebanoni uliingia miaka 600 baada ya kuwepo kwa Ukristo nchini humo. Kwa sasa nafasi ya Rais wa Lebanoni iko wazi tangu mwezi Oktoba 2022 baada ya Rais Michel Aun kuachia nafasi hiyo ya Urais. Bunge halikuweza kumchagua Rais kwa sababu mtu aliyegombea nafasi hiyo hakupata wingi wa kura zinazotakiwa kikatiba.
Kanisa la Maronite la Lebanoni linakadiriwa pia kuwa na idadi ya waumini ambao ni sawa na 30% ya wananchi wote wa Lebanoni. Waislamu wa madhehebu ya Shia wana waumini ambao ni sawa na 27% ya wananchi wa Lebanoni. Vile vile, Waislamu wa madhehebu ya Sunni wana waumini ambao ni sawa na 27% ya wananchi wote wa Lebanoni. Greek Orthodox Church ni 8%, Melkite Christian ni 5% na Waprotestanti ni 1% huku kukibakia idadi ndogo sana waabudu wa dini za asili za Kikaanani. Dini za Kikaanani zilikuwepo tangu wakati wa Ibrahimu kwani pia hata yeye alikuwa muumini wa dini hizo kabla hajapewa wito na Mungu (Mwanzo 12).
Kwa ujumla, ni wazi kuwa nchi ya Lebanoni ina idadi kubwa zaidi ya Wakristo kuzidi hata nchi ya Israeli ambayo asilimia kubwa ya wananchi wake ni wa dini za Kiyahudi na Kiislamu. Vizuri watu wakaelewa kuwa hata Wapalestina wengi wao ni Wakristo. Kwa hiyo ni makosa sana kwa watu kufikiri Uarabu ni Uislamu na Uislamu pia ni Ukristo. Kuna Wakristo wengi sana katika nchi za Kiarabu hasa Lebanoni, Syria na Misri.