HEMBU LEO TUPITE KWENYE HUU MZOZO WA ISRAEL NA HAMASI HUKO PALESTINA
Yahya Sinwar: Kiongozi wa Hamas ni nani?
Mwandishi wetu
Jeshi la Israel linasema linachunguza iwapo vikosi vyake katika Ukanda wa Gaza vimemuua kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, mpangaji mkuu wa shambulio la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel na mtu anayesakwa zaidi nchini humo.
Sinwar – ambaye ana nywele nyeupe- alitoweka mwanzoni mwa vita vilivyosababishwa na shambulio hilo, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na wengine 251 walichukuliwa mateka.
Hilo halikuwa jambo la kushangaza, kwani maelfu ya wanajeshi wa Israel wakisaidiwa na ndege zisizo na rubani, vifaa vya kielektroniki vya kusikiliza na watoa habari nyanjani, walijaribu kumsaka.
“Yahya Sinwar ndiye kamanda … na ni mtu aliyekufa,” msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) alitangaza Admiral Daniel Hagari mara baada ya shambulio la Israeli.
“Shambulio hili la kuchukiza liliamuliwa na Yahya Sinwar,” Mkuu wa IDF Herzi Halevi alisema. “Kwa hiyo, yeye na wote walio chini yake ni wafu wanaotembea.”
Hao ni pamoja na Mohammed Deif, kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas, Brigedi ya Izzedine al-Qassam, ambaye IDF ilisema aliuawa katika shambulio la anga huko Gaza mwezi Julai.
Hugh Lovatt, mshirika mkuu wa sera katika Baraza la Uropa la Mahusiano ya Kigeni (ECFR), anaamini Deif ndiye alihusika na upangaji wa shambulio la Oktoba 7 kwa sababu ilikuwa operesheni ya kijeshi, lakini kwamba Sinwar “alikuwa sehemu ya kundi ambalo lilipanga na kuishawishi”.
Kabla ya tangazo la Alhamisi, IDF iliamini kuwa Sinwar alikuwa amejificha chini ya ardhi, akijificha kwenye mahandaki mahali fulani chini ya Gaza na walinzi wake, akiwasiliana na watu wachache sana kwa hofu kwamba ishara zake za mawasiliano kupitia njia ya elektroniki itafuatiliwa na kupatikana.
Licha ya hayo, alitajwa kuwa kiongozi wa jumla wa Hamas kufuatia mauaji ya Ismail Hanieyh mjini Tehran mwezi Julai na aliripotiwa kuwasiliana na maafisa wa Hamas wenye makao yake nchini Qatar waliohusika katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka mapema mwezi huu.
Unaweza Pia Kusoma
Nini kimewapata viongozi mashuhuri wa Hamas?
2 Agosti 2024
Wafahamu viongozi mashuhuri wa sasa wa Hamas wanaosakwa na Israel
16 Oktoba 2023
Mauaji ya kiongozi wa Hamas yanazusha hofu kubwa ya vita
3 Januari 2024
Malezi na kukamatwa kila mara
Sinwar, 61, anayejulikana sana kama Abu Ibrahim, alizaliwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis katika mwisho wa kusini wa Ukanda wa Gaza. Wazazi wake walitoka Ashkelon lakini wakawa wakimbizi baada ya kile Wapalestina wanachokiita “al-Naqba” (Janga) – kuhamishwa kwa wingi kwa Wapalestina kutoka kwa nyumba za mababu zao huko Palestina katika vita vilivyofuata kuanzishwa kwa taifa la Israeli mnamo 1948.
Alisoma katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Khan Younis kisha akahitimu na shahada ya kwanza ya lugha ya Kiarabu kutoka Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza.
Wakati huo, Khan Younis alikuwa “ngome” ya kuunga mkono Muslim Brotherhood, anasema Ehud Yaari, mwanazuoni wa Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Karibu, ambaye alimhoji Sinwar gerezani mara nne.
Kundi hilo la Kiislamu “lilikuwa vuguvugu kubwa kwa vijana wanaokwenda misikitini katika umaskini wa kambi ya wakimbizi”, Yaari anasema, na baadaye lingechukua umuhimu sawa na huo kwa Hamas.
Sinwar alikamatwa kwa mara ya kwanza na Israel mwaka 1982, akiwa na umri wa miaka 19, kwa “shughuli za Kiislamu” na kisha akakamatwa tena mwaka 1985. Ilikuwa ni wakati huu ambapo alipata kuwa karibu na mwanzilishi wa Hamas, Sheikh Ahmed Yassin.
Wawili hao wakawa “wandani wa karibu sana”, anasema Kobi Michael, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Mafunzo ya Usalama wa Kitaifa huko Tel Aviv. Uhusiano huu na kiongozi wa kiroho wa shirika hilo baadaye ungempa Sinwar “athari ya kipekee” ndani ya harakati, Michael anaongeza.
Miaka miwili baada ya Hamas kuanzishwa mwaka 1987, alianzisha shirika la usalama wa ndani la kundi hilo linaloogopwa, al-Majd. Bado alikuwa na miaka 25 tu.
Al-Majd ilipata umaarufu mbaya kwa kuwaadhibu wale wanaotuhumiwa kwa makosa ya maadili – Michael anasema alilenga maduka ambayo yalikuwa na “video za ngono” – pamoja na kuwinda na kuua mtu yeyote anayeshukiwa kushirikiana na Israeli.
Yaari anasema alihusika na “mauaji mengi ya kikatili” ya watu wanaoshukiwa kushirikiana na Israel. “Baadhi yao kwa mikono yake mwenyewe na alijivunia hilo, akiongea nami na wengine kuhusu hilo”
Kulingana na maafisa wa Israel, baadaye alikiri kumwadhibu mshukiwa kuwa mtoa habari kwa kumfanya nduguye mtu huyo amzike akiwa hai, na kumaliza kazi hiyo kwa kutumia kijiko badala ya sepeto
“Yeye ni aina ya mtu ambaye anaweza kukusanya karibu naye wafuasi, mashabiki – pamoja na wengi ambao wanamuogopa na hawataki kupigana naye,” Yaari anasema.
Mnamo 1988, Sinwar alidaiwa kupanga utekaji nyara na mauaji ya wanajeshi wawili wa Israeli. Alikamatwa mwaka huo huo, akahukumiwa na Israel kwa mauaji ya Wapalestina 12 na kuhukumiwa vifungo vinne vya maisha.
Miaka gerezani
Sinwar ametumia sehemu kubwa ya maisha yake ya utu uzima – zaidi ya miaka 22 – katika magereza ya Israeli, kutoka 1988 hadi 2011. Muda wake huko, baadhi yake katika kifungo cha upweke, unaonekana kuwa ulimfanya awe na msimamo mkali zaidi.
“Alifanikiwa kulazimisha mamlaka yake bila huruma, kwa kutumia nguvu,” anasema Yaari. Alijiweka kama kiongozi miongoni mwa wafungwa, akijadiliana kwa niaba yao na wakuu wa magereza na kutekeleza nidhamu miongoni mwa wafungwa.
Tathmini ya serikali ya Israeli kuhusu Sinwar wakati alipokuwa gerezani ilielezea tabia yake kama “katili, mwenye mamlaka, ushawishi na uwezo usio wa kawaida wa uvumilivu, ujanja na kuridhika na na machache… Huweka siri hata ndani ya jela miongoni mwa wafungwa wengine… Ana uwezo kubeba umati wa watu”.
Tathmini ya Yaari juu ya Sinwar, iliyojengwa juu ya nyakati walizokutana, ilikuwa kwamba yeye ni ‘mtu mwenye upotofu wa kiakili’ au ‘psychopath’. “[Lakini] kusema kuhusu Sinwar, ‘Sinwar ni mtu mwenye tatizo la kiakili,,’ itakuwa kosa,” anasema, “kwa sababu basi utakosa sura hii ya ajabu, tata”.
Yeye, ni “mjanja sana, mwerevu – mtu anayejua kuwasha na kuzima aina ya haiba ya kibinafsi”.
Wakati Sinwar alipomwambia Israeli lazima iangamizwe na kusisitiza kuwa hakuna mahali pa Wayahudi huko Palestina, “alikuwa akitania, ‘Labda tutakusaza wewe'”.
Akiwa mfungwa Sinwar alikuwa amejua vizuri Kiebrania, akisoma magazeti ya Israeli. Yaari anasema Sinwar siku zote alipendelea kuzungumza naye Kiebrania, ingawa Yaari alikuwa anajua Kiarabu.
“Alitafuta kuboresha Kiebrania,” Yaari anasema. “Nadhani alitaka kufaidika na mtu ambaye alizungumza Kiebrania cha juu zaidi kuliko wasimamizi wa gereza.”
Sinwar aliachiliwa huru mwaka 2011 kama sehemu ya makubaliano ambayo yalishuhudia wafungwa 1,027 wa Wapalestina na Waarabu wa Israeli wakiachiliwa kutoka jela kwa kubadilishana mateka mmoja wa Israel, mwanajeshi wa IDF Gilad Shalit.
Shalit alikuwa ameshikiliwa mateka kwa miaka mitano baada ya kutekwa nyara na – miongoni mwa wengine – kaka yake Sinwar, ambaye ni kamanda mkuu wa kijeshi wa Hamas. Tangu wakati huo Sinwar ametoa wito wa utekaji nyara zaidi wa wanajeshi wa Israel.
Kufikia sasa, Israel ilikuwa imemaliza kukalia kwa mabavu Ukanda wa Gaza na Hamas ilikuwa inaongoza, baada ya kushinda uchaguzi na kisha kuwaondoa wapinzani wake, chama cha Fatah cha Yasser Arafat, kwa kuwatupa wanachama wake wengi kutoka juu ya majengo marefu.
Nidhamu ya ‘kikatili’
Sinwar aliporudi Gaza, alikubaliwa mara moja kama kiongozi, Michael anasema. Mengi ya haya yalihusiana na heshima yake kama mwanachama mwanzilishi wa Hamas ambaye alijitolea kwa miaka mingi ya maisha yake katika magereza ya Israeli.
Lakini pia, “watu walimwogopa tu – huyu ni mtu aliyeua watu kwa mikono yake,” Michael anasema. “Alikuwa mkatili sana, mchokozi na mwenye haiba kwa wakati mmoja.”
“Yeye si mzungumzaji,” anasema Yaari. “Anapozungumza na umma, ni kama mtu kutoka kwa magenge ya uhalifu.”
Yaari anaongeza kuwa mara baada ya kutoka gerezani, Sinwar pia alianzisha muungano na Brigedi za Izzedine al-Qassam na mkuu wa majeshi Marwan Issa.
Mnamo 2013, alichaguliwa kuwa mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas katika Ukanda wa Gaza, kabla ya kuwa mkuu wake mnamo 2017.
Kaka mdogo wa Sinwar Mohammed pia aliendelea na jukumu kubwa katika Hamas. Alidai kuwa alinusurika katika majaribio kadhaa ya mauaji ya Israel kabla ya kutangazwa kuwa amekufa na Hamas mwaka 2014. Ripoti za vyombo vya habari tangu wakati huo zimeibuka zikidai kuwa anaweza kuwa bado yuko hai, akifanya kazi katika mrengo wa kijeshi wa Hamas kujificha kwenye mahandaki ya chini ya Gaza na huenda hata alishiriki katika shambulio la Oktoba 7.
Sinwar ana sifa ya ukatili na jeuri ilimfanya apewe jina la utani la The Butcher of Khan Younis.(Muuaji wa Khan Younis)
“Yeye ni mtu ambaye anaweka nidhamu ya kikatili,” anasema Yaari, “Watu walijua katika Hamas na bado wanafanya hivyo – ikiwa utaasi Sinwar, unaweka maisha yako hatarini.”
Anatajwa kuhusika na kuwekwa kizuizini, kuteswa na kumuua kamanda wa Hamas aitwaye Mahmoud Ishtiwi mwaka 2015 ambaye alituhumiwa kwa ubadhirifu na ulawiti.
Mnamo mwaka wa 2018, katika mkutano na vyombo vya habari vya kimataifa, aliashiria uungaji mkono wake kwa maelfu ya Wapalestina kuvunja uzio wa mpaka unaotenganisha Ukanda wa Gaza na Israel kama sehemu ya maandamano ya kupinga Marekani kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem.
Baadaye mwaka huo alidai kunusurika katika jaribio la mauaji lililofanywa na Wapalestina watiifu kwa mamlaka hasimu ya Palestina (PA) katika Ukingo wa Magharibi.
Hata hivyo pia ameonyesha upande wake wa kutambua uhalisia wa mambo, kuunga mkono usitishaji vita wa muda na Israel, kubadilishana wafungwa, na maridhiano na Mamlaka ya Palestina. Hata alikosolewa na baadhi ya wapinzani kuwa mwenye msimamo wa wastani, Michael anasema.
Uhusiano wa karibu na Iran
Wengi katika taasisi ya ulinzi na usalama ya Israeli wanaamini kuwa lilikuwa kosa kubwa kumwachilia Sinwar kutoka gerezani kama sehemu ya kubadilishana wafungwa.
Waisraeli wanahisi waliingizwa katika hali ya uwongo ya usalama kwa imani potofu kwamba kwa kutoa motisha ya kiuchumi kwa Hamas na vibali zaidi vya kazi, harakati hiyo ingepoteza hamu yake ya vita. Hii, bila shaka, iligeuka kuwa hesabu mbaya sana.
“Anajiona kama mtu anayekusudiwa kuikomboa Palestina -sio kuhusu kuboresha hali ya uchumi, huduma za kijamii kwa Gaza,” anasema Yaari. “Siyo yeye.”
Mnamo mwaka wa 2015, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilimtaja rasmi Sinwar kama “Gaidi Maalum”. Mwezi Mei 2021 mashambulizi ya anga ya Israel yalilenga nyumba na ofisi yake katika Ukanda wa Gaza. Mnamo Aprili 2022, katika hotuba ya televisheni, alihimiza watu kushambulia Israeli kwa njia yoyote inayopatikana.
Wachambuzi wamemtambua kama mtu muhimu anayeunganisha ofisi ya kisiasa ya Hamas na mrengo wake wenye silaha, Brigedi ya Izzedine al-Qassam, ambayo iliongoza mashambulizi ya Oktoba 7 kusini mwa Israeli.
Mnamo tarehe 14 Oktoba 2023, msemaji wa jeshi la Israeli, Lt Kanali Richard Hecht, alimwita Sinwar “uso wa uovu”. Aliongeza: “Mtu huyo na timu yake yote wako machoni mwetu. Tutamfikia mtu huyo.”
Sinwar pia yuko karibu na Iran. Ushirikiano kati ya nchi ya KiShia na shirika la Waarabu wa Sunni sio jambo la wazi, lakini wote wawili wana lengo la kumaliza taifa la Israeli na “kuikomboa” Jerusalem kutoka kwa utawala wa Israel.
Wamekuja kufanya kazi bega kwa bega. Iran inafadhili, inatoa mafunzo na silaha kwa Hamas, kusaidia kujenga uwezo wake wa kijeshi na kukusanya shehena ya maelfu ya makombora, ambayo inatumia kulenga miji ya Israel.
Sinwar alitoa shukrani zake kwa uungwaji mkono huo katika hotuba yake mwaka 2021. “Kama si Iran, Harakati za Palestina hazingekuwa na uwezo wake wa sasa.”
Bado kumuua Sinwar itakuwa zaidi ya “ushindi wa uhusiano mwema” kwa Israeli kuliko kuweza kuathiri harakati, Lovatt anasema.
Mashirika yasiyo ya serikali huwa yanafanya kazi kama kichwa cha mnyama aitwaye hydra – kamanda mmoja au kiongozi mkuu anaondolewa na nafasi yao kuchukuliwa haraka na mwingine. Mrithi wao wakati mwingine anakosa uzoefu au uaminifu sawa lakini shirika bado linaweza kujitengeneza upya kwa namna fulani.
“Ni wazi, itakuwa hasara,” anasema Lovatt, “lakini nafasi yake itazibwa na kuna miundo inayotumika kufanya hivyo. Sio kama kumuua Bin Laden. Kuna viongozi wengine wakuu wa kisiasa na kijeshi ndani ya Hamas.”
Labda swali kubwa zaidi linabaki kuwa hili – nini kitatokea kwa Gaza wakati Israeli inapomaliza kampeni yake ya kijeshi ya kutokomeza Hamas, na ni nani atakayeongoza?
Na je, wanaweza kuizuia isije ikawa tena sehemu ya kuzindua mashambulizi dhidi ya Israeli, na hivyo kuibua aina ya adhabu na uharibifu mkubwa tunaouona sasa.
Pichani ni
Yahya Sinwar
Yahya Sinwar
Kiongozi wa kiroho.