Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso inayoongozwa na Kapteni Ibrahim Traore imevunja serikali ya kiraia na kumwondoa madarakani Waziri Mkuu wa mpito, Apollinaire Joachim Kyelem de Tambela, kwa mujibu wa amri iliyotangazwa siku ya Ijumaa.
Amri hiyo haikutaja sababu za kufutwa kwa Tambela, ambaye aliteuliwa kushika nafasi hiyo mara baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomweka Traore madarakani mnamo Septemba 2022. Tukio hili ni sehemu ya wimbi la mapinduzi ya kijeshi yaliyotikisa eneo la Sahel katika miaka ya karibuni.
Kwa mujibu wa amri hiyo, mawaziri waliokuwemo katika serikali iliyovunjwa wataendelea kutekeleza majukumu yao hadi baraza jipya la mawaziri litakapoundwa.
Burkina Faso imeendelea kukumbwa na mashambulizi ya waasi wa Kiislamu wenye uhusiano na al-Qaeda na Islamic State tangu waasi hao walipoingia nchini humo kutoka Mali miaka karibu kumi iliyopita.
Traore alipochukua madaraka, aliahidi kushughulikia hali ya usalama kwa ufanisi zaidi kuliko viongozi wa awali, lakini wachambuzi na makundi ya haki za binadamu wanasema kuwa usalama umedhoofika zaidi huku utawala wake ukikandamiza wapinzani na uhuru wa kujieleza.