Baraza la Usalama la Taifa la Iran limesitisha utekelezaji wa sheria ya hijabu na kutokuwa na mahusiano yoyote ya ngono kabla ya ndoa, ambayo ilikuwa ianze kutekelezwa siku ya Ijumaa.
Sheria mpya iliyopendekezwa ambayo ingetoa adhabu kali zaidi kwa wanawake na wasichana kwa kutofunika nywele zao, kuonyesha mapaja au sehemu ya chini ya miguu, ilikuwa imekosolewa vikali na wanaharakati wanaotetea haki za kibinadamu.
Kanuni kali za mavazi zilizowekwa kwa wanawake na wasichana, ambazo zimechukuliwa kama kipaumbele cha usalama wa taifa na watawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa miongo kadhaa, zimesababisha maandamano siku za nyuma.
Chini ya sheria hiyo mpya, watu wanaorudia makosa na yeyote aliyekejeli sheria hizo atakabiliwa na faini kubwa zaidi na kifungo cha muda mrefu cha hadi miaka 15 jela.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yalionyesha wasiwasi wake, ambapo Amnesty International ilisema mamlaka za Irani zinatafuta kuimarisha mfumo wa ukandamizaji ambao tayari unakera wengi.
Wakati wa uchaguzi wa rais mwezi Julai, mgombea wa wakati huo Pezeshkian alikosoa waziwazi jinsi wanawake wa Iran wanavyotendewa kuhusu suala la kuvaa hijabu.
Aliahidi kutoingilia maisha yao binafsi, msimamo ambao uliwagusa Wairani wengi haswa kutoka kwa kundi la vijana waliokatishwa tamaa na udhibiti mkali wa Serikali.
Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, vijana wengi wa kike wa Kiirani wamevua hijabu zao kwa ukaidi hadharani, wakipinga mamlaka ya Serikali.