Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ,John Heche amesema ukimya wake yeye binafsi na wenzake (waliokaa kimya) ndani ya chama hicho unatokana na kile alichokieleza ni kuepusha mpasuko zaidi ndani ya chama hicho hususani katika kipindi hiki ambacho chama hicho kipo kwenye mchakato wa ndani wa uchaguzi
Kupitia chapisho lake aliloweka kwenye mitandao yake binafsi ya kijamii Heche amesema kama Taifa kwa ujumla tunalo jukumu la msingi la kuhakikisha nchi inapata chama mbadala na serikali mbadala itakayokuwa na wajibu wa msingi wa kuwatumikia watu na kuwaondoa Watanzania katika dimbwi la umaskini uliodumi kwa takribani miaka 63 ya uhuru
Amesema Watanzania wana shauku ya kuona serikali na chama cha siasa kitakachopinga rushwa kwa vitendo na bila aibu, chama cha siasa kinachochukia umaskini, kitakachoongoza na kutumia raslimali za Taifa kwa kuendeleza maisha ya Watanzania na si vinginevyo
“Hata hivyo katika wakati muafaka na muda sio mrefu nitazungumza na kutoa muelekeo wangu katika jambo hili kubwa” -Heche
Hata hivyo, Heche ambaye pia ni Mbunge wa zamani wa jimbo la Tarime vijijini kupitia CHADEMA amesema amepokea jumbe nyingi kwa njia tofauti ikiwemo simu kuhusiana na ukimya wake huku wengi wanaomtafuta wakimuomba aseme jambo kuhusiana na kile kinachoendelea katika chama hicho
“Nimepata jumbe nyingi, simu nyingi, nawahakikishia Watanzania na wanachama wa CHADEMA kwamba nimewasikia na nitazungumza” -Heche
Ikumbukwe, miongoni mwa jumbe na mijadala iliyoko sana kwenye mitandao ya kijamii kwa sasa (inayomuhusu John Heche) ni ile inayomuomba kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara.