
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ametoa onyo kali kwa Afrika Kusini, akimtuhumu Rais Cyril Ramaphosa na serikali yake kwa kupotosha ukweli kuhusu mgogoro unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Kagame ameonesha kuwa Rwanda iko tayari kwa makabiliano ikiwa ni lazima.
“Kile kinachosemwa na maafisa wa Afrika Kusini na Rais Ramaphosa kuhusu mazungumzo tuliyofanya wiki hii ni mchanganyiko wa upotoshaji, mashambulizi ya makusudi, na hata uongo,” amesema Kagame katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa X.
Matamshi haya yameibuka siku chache baada ya vifo vya wanajeshi 13 wa Afrika Kusini waliokuwa wakihudumu chini ya ujumbe wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika DRC (SAMIDRC).
Vifo hivyo vimeongeza shinikizo la kisiasa na kijeshi jijini Pretoria, huku serikali ya Afrika Kusini ikijitetea kuhusu kuingilia mgogoro wa muda mrefu wa DRC, wakati uhusiano wake na Rwanda ukiendelea kuzorota.
Maafisa wa Afrika Kusini wameilaumu Rwanda na waasi wa M23 kwa kuchochea machafuko yanayoendelea, wakidai kuwa mashambulizi yao yalisababisha vifo vya wanajeshi wao. Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Ronald Lamola, amesema kuwa wanashirikiana na Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kushinikiza kusitishwa kwa mapigano mara moja.
Kwa upande wake, Rais Kagame amepuuzilia mbali jukumu la Afrika Kusini katika juhudi za kuleta amani, akidai kuwa SAMIDRC si ujumbe wa kulinda amani bali ni jeshi linalopendelea upande mmoja likiunga mkono serikali ya DRC.
Kagame ameendelea kuituhumu SAMIDRC kwa kushirikiana na kundi la Forces Démocratiques de Libération du Rwanda (FDLR), ambalo lina mizizi ya kihistoria na wahusika wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
“FDLR inatishia Rwanda huku pia ikitangaza kutaka kupeleka vita ndani ya Rwanda yenyewe,” amesema Kagame.
Amedai kuwa SAMIDRC imechukua nafasi ya Jeshi la Kikanda la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF), ambalo alisema ndilo pekee lenye mamlaka halali ya kulinda amani katika eneo hilo.
Kagame amekanusha madai kwamba Ramaphosa alimpa onyo lolote, akisema: “Rais Ramaphosa hajawahi kunipa onyo la aina yoyote, labda alitoa katika lugha yake ya nyumbani ambayo siielewi.”
Badala yake, amedai kuwa Ramaphosa alimuomba msaada wa vifaa vya msingi kama umeme, chakula, na maji kwa wanajeshi wa Afrika Kusini, na Rwanda ilikuwa tayari kusaidia.
Kagame pia amedai kuwa Ramaphosa alikiri binafsi kuwa M23 haikuhusika na vifo vya wanajeshi wa Afrika Kusini, bali vikosi vya Jeshi la DRC (FARDC) ndilo lililohusika.
“Kama Afrika Kusini inataka kuchangia suluhu ya amani, hilo ni jambo jema. Lakini kama wanataka makabiliano, Rwanda itashughulikia hali hiyo ipasavyo wakati wowote,” amesema Kagame.
Mapema, Ramaphosa alitoa taarifa akisema kuwa mgogoro wa DRC umesababishwa na ongezeko la mashambulizi kutoka kwa waasi wa M23 na Jeshi la Rwanda (RDF).
Alisema hali ya usalama mashariki mwa DRC ni “tete, hatari, na isiyotabirika” na akaahidi msaada kwa familia za wanajeshi waliouawa pamoja na wale waliojeruhiwa.
Ramaphosa alisisitiza kuwa Afrika Kusini haipo vitani na nchi yoyote na kwamba uwepo wake DRC ni sehemu ya juhudi za kimataifa na kikanda za kulinda amani.
“Jeshi la Afrika Kusini lipo DRC kwa lengo la kulinda raia na kuimarisha utulivu katika eneo hilo lililoathiriwa na vita vya muda mrefu,” alisema Ramaphosa.
Alihimiza pande zote kuheshimu makubaliano ya amani, ikiwemo Mchakato wa Luanda, na kuheshimu mipaka ya DRC. Pia alikaribisha azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa kwa uhasama na kuondolewa kwa majeshi ya kigeni katika ardhi ya DRC.