HABARI KUU
Polisi wa Transmara, Kaunti ya Narok Nchini Kenya, wanachunguza kisa kimoja cha Afisa wa kitengo cha RDU (Rapid Deployment Unit), Dennis Imai ambaye alifyatua risasi moja hewani alipodaiwa deni la Pombe aliyokunywa katika baa moja.
Afisa huyo ambaye amewekwa katika kambi ya RDU kijiji cha Enkorika, inasemekana alilimbikizia bili ya KSh. 2, 220 kutokana na chupa kadhaa za bia aliyokuwa ameinywa katika baa hiyo iliyoko Lolgorian.
Aprili 7, 2024 afisa huyo alirudi katika baa hiyo na mhudumu aliyekuwa amemuuzia Kinywaji, Bi Jackline Jemeli aliulizia deni hilo na alimshurutisha Imai amlipe kwa kumpokonya simu yake.
Mashuhuda wanasema baada ya mabishano ya muda mfupi, Afisa huyo ambaye alikuwa amevaa kiraia aliondoka na alirejea na Bodaboda baada ya dakika 30 akiwa amevalia sare kamili za Polisi, huku akiwa amejihami na bunduki.
Wanasema, ““alidai simu yake kwa nguvu na mhudumu alipokataa kumpa, alifyatua risasi moja na kisha kuondoka na bodaboda huyo aliyekuwa amesimama mita chache,” na hakuna mtu aliyejeruhiwa katika tukio hilo.