HABARI KUU
Rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani, Ali Bongo pamoja na wanawe wawili wameanza mgomo wa kula wakilalamikia “vitendo vya mateso na ukatili” wanavyofanyiwa, mawakili wa familia hiyo wamesema.
Bongo aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti mwaka jana, muda mfupi baada ya kushinda kura za urais.
Kisha alizuiliwa nyumbani kwake katika mji mkuu, Libreville, pamoja na wanawe wawili, Jalil na Bilal.
Utawala wa kijeshi pia uliwaweka mkewe, Sylvia Bongo na mwanawe mkubwa Noureddin gerezani, wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Katika taarifa yao, mawakili wao wamedai kuwa Noureddin na Sylvia walipigwa na kunyongwa wakiwa kizuizini.
Pia wanadai kuwa Noureddin aliteswa, kuchapwa viboko na “hata kupigwa kwa shoti ya umeme.”
Serikali ya Gabon bado haijasema lolote kuhusu madai hayo.
Ali Bongo mwenye umri wa miaka 64, aliongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu 2009 alipomrithi baba yake ambaye alikuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.
Mawakili wa familia hiyo wanasema pia wamewasilisha malalamiko katika mahakama ya Haki za Binadamu, Paris, Ufaransa, wiki moja kabla ya kiongozi wa sasa wa serikali ya Gabon, Brice Oligui Nguema kuzuru Ufaransa.