MICHEZO
Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo ameweka wazi dhamira na malengo yake ya kuhakikisha anatwaa taji la FA msimu huu 2023/24.
Azam FC itacheza na Coastal Union keshokutwa Jumamosi (Mei 18) Katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kuwania nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazi za klabu Tanzania Bara.
Akizungumza jijini humo, Dabo amekiri mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini dhamira yao ni kutinga fainali na kubeba taji hilo msimu huu.
Kocha huyo amesema ameifuatilia Coastal Union na kugundua ubora na udhaifu wao, hivyo atatumia udhaifu wa wapinzani wake kupata ushindi katika mechi hiyo.
“Kikubwa sisi tunahitaji taji la FA, tunajua tuna mechi ngumu hadi kufika fainali, lakini naamini tutapambana kuhakikisha tunashinda kila mechi tutwae taji hilo na kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa mwakani,” amesema.
Azam FC imetinga Nusu Fainali baada ya kuifunga Namungo FC mabao 4-1 katika mechi ya Robo Fainali ya michuano hiyo.