MICHEZO
Klabu ya Liverpool imemtangaza rasmi aliyekuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Feyenoord ya nchini Uholanzi Arne Slot, kuwa mrithi wa Jurgen Klopp aliyeondoka klabuni hapo juzi Jumapili (Mei 19).
Slot alitarajiwa kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Liverpool kabla ya kutangazwa na Uongozi wa Klabu hiyo, kwani aliwahi kuwathibitishia Waandishi wa Habari nchini kwao kuwa atafanya kazi Anfield kuanzia msimu ujao.
Slot ataanza kazi kama Kocha Mkuu wa The Reds Juni Mosi, akitarajiwa kuendeleza mazuri yaliyoachwa na Klopp ambaye alikuwa na mafanikio makubwa tangu alipotua klabuni hapo mwaka 2015.
Kabla ya kutangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Liverpool, Slot alitoa neno la shukurani kwa Mashabiki wa Feyenoord akisema: “Hakika si uamuzi rahisi kufunga mlango nyuma yako katika klabu ambayo umepitia matukio mengi ya ajabu na kufanya kazi kwa mafanikio kwa kushirikiana na watu wengi.”
“Lakini kama mwanamichezo, nimeipokea kwa moyo mkunjufu nafasi ya kuwa sehemu ya makocha wa Ligi ya England, na katika moja ya klabu kubwa duniani, ilikuwa vigumu kwangu kuikataa fursa hii.”