Watu 80 wamefariki dunia baada ya Boti kuzama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rais wa nchi hiyo amethibitisha Felix Tshisekedi.
Maafa hayo yalitokea jana Jumatano kwenye Mto, Kilomita 70 kutoka Mji wa Mushie katika Jimbo la Maï-Ndombe karibu na mpaka wa nchi jirani ya Congo-Brazzaville.
Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii, Rais Félix Tshisekedi alisema amehuzunishwa na kifo cha raia wake.
Rais huyo alisema walioathiriwa watapata usaidizi na pia akaagiza uchunguzi ufanyike kubaini kilichosababisha maafa hayo.
” Rais wa Jamhuri ya Congo anatoa wito wa uchunguzi kuhusu sababu za kweli za tukio hili la kusikitisha, ili kuzuia maafa kama haya yasijitokeze tena katika siku zijazo,” ofisi ya rais ilisema kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter.
Ajali mbaya za boti ni za kawaida nchini DR Congo, ambapo boti mara nyingi hujaa abiria ambao ni nadra kupewa jaketi za usalama na mara nyingi hawawezi kuogelea.