Jana, Rais Cyril Ramaphosa aliapishwa kuendelea kuongoza Taifa la Afrika Kusini kwa kipindi kingine cha miaka mitano huku mwenza wake, Tshepo Motsepe akiwa mwenye furaha kubwa katika sherehe zilizoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Tshepo Motsepe ni nani? Mwanamke huyu aliyezaliwa Juni 17, 1953 ni tabibu (physician) na mfanyabiashara. Yeye ni dada mkubwa wa Bridgette Radebe na Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Dkt. Patrice Motsepe ambaye pia ndiye mmiliki wa klabu ya Mamelodi Sundowns.
Bilionea Dkt. Patrice Motsepe alizaliwa Januari 28, 1962. Tangu Machi 2021, amekuwa Rais wa CAF. Patrice ndiye mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wa African Rainbow Minerals, kampuni inayojihusisha na biashara ya madini mbalimbali ikiwemo dhahabu.
Ni mjumbe wa bodi kadhaa za kampuni mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti asiye mtendaji wa Harmony Gold, kampuni ya 12 kwa ukubwa duniani katika kuchimbaji wa dhahabu. Pia na makamu mwenyekiti wa kampuni nyingine matata ya Sanlam. Motsepe pia yumo kwenye Bodi ya Wadhamini ya Jukwaa la Kiuchumi la Dunia.