Rais William Ruto ametangaza kusitisha kusaini Muswada wa Sheria ya Fedha na kuagiza urejeshwe Bungeni kwaajili ya kufanyiwa maboresho kadhaa kabla ya Wabunge kwenda mapumziko.
Katika kikao na waandishi wa habari siku moja baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa nchini kupinga mswada huo ,Ruto pia ametangaza hatua mbalimbali za kupunguza mgao wa fedha za matumizi katika Ofisi ya Rais na idara nyingine za serikali ikiwemo bunge .
Ruto amesema serikali italazimika kuanza upya mchakato wa kutoa mapendekezo ya kukusanya fedha utakaohusisha wadau kutoka sekta mbali mbali .Katika kikao hicho rais Ruto alianza kwa kutaja baadhi ya hatua ambazo serikali imechukua tangu ilipotwa usukani kupunguza gharama ya maisha ikiwemo kupunguza bei ya unga,mbolea na mafuta ya kupikia .
Takriban watu 22 waliuawa katika maandamano ya Jumanne, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNHRC) inayofadhiliwa na serikali.
“Baada ya kutafakari juu ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu mswada wa fedha wa 2024 na kusikiliza kwa makini watu wa Kenya, ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na na mswada wa fedha wa 2024, nakubali na kwa hivyo sitatia saini mswada wa fedha wa 2024 na utaondolewa baadaye. Wananchi wamesema.” Alisema rais Ruto