Rais wa Marekani, Joe Biden amewatoa wasiwasi wafuasi wa chama chake cha Demokrati wanaoonesha wasiwasi baada kutofanya vuzuri kwenye mdahalo na mpinzani wake, Donald Trump huku umri ukitajwa kwamba amechoka, akisema ana hakika atashinda tena uchaguzi wa Novemba.
“Ninajua mimi si kijana, kusema kweli,” alisema katika mkutano huko North Carolina, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada mpambano na mpinzani wake wa chama cha Republican, Donald Trump.
“Sitembei kwa wepesi kama nilivyokuwa zamani… Sijadili kwa harakaharaka kama nilivyokuwa nikijadili,” alikiri. “Lakini ninachojua, kwa hakika, ninasema ukweli na ninajua vizuri jinsi ya kufanya kazi hii (ya urais).”
Biden, 81, amesema anaamini kwa “moyo mmoja” kwamba anaeweza kuhudumu muhula mwingine bila wasiwasi wowote huku umati wa watu waliokuwa wakimshangilia mjini Raleigh wakisema kwa sauti “minne mingine tena”, kumaanisha apewe miaka minne zaidi ya kuongoza Taifa hilo kubwa.
Wakati huohuo, Trump amefanya mkutano huko Virginia saa chache baadaye, ambapo amesifia “ushindi wake mkubwa” katika mdahalo huo, ambao CNN ilisema ulitazamwa na watu milioni 48 kwenye televisheni na mamilioni zaidi mtandaoni.
“Tatizo la Joe Biden sio umri wake,” Trump mwenye umri wa miaka 78 alisema. “Ni uwezo wake. Hana uwezo kabisa.”
Rais huyo wa zamani alisema haamini pia uvumi kwamba Biden angejiondoa katika kinyang’anyiro hicho.