Kauli ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia na Teknolojia ya Habari Nape Moses Nnauye aliyoitoa leo Julai 16,2024 akidai CCM lazima ishinde kwa njia yoyote kwenye uchaguzi, imemuibua Mtetezi wa haki za Binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa ambaye ni Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu Tanzania (THRDC) akimtaka Waziri Nape kuomba radhi kwa wananchi kutokana na kauli yake.
“Matokeo ya kura siyo lazima yawe yale ya kwenye box, inategemea nani anahesabu na nani anatangaza. Unajua kuna mbinu nyingi za uchaguzi, Kuna halali, nusu halali na haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi ukimaliza unasema Mungu nisamehe” alisema Nape.
Wakili Olengurumwa Amesema kuwa amesikitishwa na kauli hiyo kwani inakinzana na mtazamo wa Rais Samia Suluhu.
“Bado tuna safari ndefu sana – Nasikitika kusikia Mhe Nape unazungumza maneno haya wakati Rais anazungumza Democracy and Four Rs. Tumetumia hela nyingi kufanya mabadiliko ya Sheria za Uchaguzi hata kama bado zinashida. Mhe Nape kwa kuwatendea haki Watanzania na kulinda your future political journey”
“tuombe radhi watanzania na kufuta kauli hii wewe mwenyewe na sio viongozi wengine ndio watoke kuikataa. Maneno haya kwa nchi zingine ingeshakuwa ni issue kubwa sana tena inaposemwa 3 months before election na kiongozi mkubwa kama wewe. Tusiposema haya na kukemea ipo siku mizimu itasema. Tunategemea pia kusikia Kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kuhusu hii kauli hii.” Amesema Olengurumwa.
Kwa upande wake katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akiwa katika mkutano wa hadhara amesema kuwa CCM imejipanga kushinda kwa haki katika uchaguzi mkuu.