Mmiliki wa mabasi ya Sauli, Solomon Sauli Mwalabila amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Miwaleni, Mlandizi mkoani Pwani majira ya saa kumi na mbili na nusu alfajiri.
Shuhuda wetu wa Pwani ameeleza kuwa ajali hiyo ilihusisha magari mawili yaliyokuwa katika sehemu moja gari namba T213 DQD aina ya Fuso.
Imeelezwa kuwa gari hilo lilipata hitilafu ya kiufundi na kuligonga gari aina ya Jeep lenye namba za usajili T466EGW alilokuwemo mmiliki wa Sauli ambapo liligonga gari jingine aina ya Howo la kubebea kokoto.
Marehemu Sauli mkazi wa Mbeya alikuwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka minne ambaye alipata michubuko na alipelekwa hospitali kabla ya kuruhusiwa.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti kituo cha afya Mlandizi.
Sauli alikuwa mmiliki mabasi ya Sauli yaliyowahi kufanya safari za Dar Es Salaam – Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa Pwani Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.