MAKALA
Tuliokuwepo tutakumbuka, mwaka ule wa 1992, kundi la Masetla, Wafanyabiashara, Wasomi na Wafanyakazi Wastaafu wa Serikali na Taasisi za Umma, lilijitokeza na kuunda chama cha siasa kiitwacho Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Masetla hao waliongozwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi Edwin Mtei. Huyu Bwana Mtei akafanywa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Chadema huku Bwana Bob Nyange Makani akifanywa kuwa Katibu Mkuu.
Safu nyingine ya waasisi wa Chadema ni pamoja na mabwana Brown Ngwilulupi, Victor Kimesera, Costa Shinganya, Edward Barongo na Philemon Ndesamburo.
Wanachama wengine waliokuwa mstari wa mbele na ambao walihudhuria Mkutano Mkuu wa kwanza wa Taifa wa Chadema ni pamoja na Bwana Freeman Mbowe, Mathias Kivigha, Francis Kabigi,Evarist Maembe na Erick Mchatta.
Chadema kikawa chama cha pili kupata usajili baada ya CCM na kabla ya NCCR-MAGEUZI na CUF. Katika hali ambayo haikutarajiwa, Mwalimu Nyerere alizisifu sera za Chadema za wakati huo.
Aidha, kwa upande wa pili, matamshi hayo ya Mwalimu Nyerere yalikiweka kwenye wakati mgumu CHADEMA. Ni baada ya chama hicho, mitaani, kugeuziwa kibao na kudaiwa kuwa ni CCM ‘B’ . Ni kwa kuwa kimesifiwa na muasisi wa CCM.
Hata hivyo, CHADEMA ya wakati huo ikiongozwa na akina Mtei, ilifanya kazi kubwa ya kujijenga na kufanikiwa kuwa chama cha kwanza kuingiza mbunge bungeni. Ni kufuatia kuitishwa kwa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kigoma Mjini.
Mchuano mkali kwenye uchaguzi huo ulikuwa ni kati ya mgombea wa Chadema, Dr. Walid Amani Kaborou dhidi ya yule wa CCM, Ndugu Suleiman Premji. Hii ilikuwa ni kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Marehemu Rajab Mbano.
Hata hivyo, katika hali ya kuonyesha kuwa chama hicho ni cha Kidemokrasia, Mwenyekiti wake Mzee Mtei alijiondoa madarakani na kumpisha Bob Makani, ambaye naye akaja kujiondoa na akamwachia Bwana Freeman Mbowe.
Ni Bwana Freeman Mbowe ambaye hadi sasa ndiye Mwenyekiti wa chama hicho.
Swali:
Chadema ya zama hizo ilikuwaje?
Jibu:
Sera za Chama hicho za mwelekeo wa Kibepari zilijibainisha kupitia Ilani ya Chama hicho.
Chadema majukwaani haikuwa na ajenda nyingi kwa wakati mmoja. Hilo liliwasaidia sana kueleweka.
Nionavyo, Chadema ya sasa ina ajenda nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuwa na ugumu wa kueleweka kwa wapiga kura, hususan walio wengi maeneo ya Vijijini.
Hata hivyo, Chadema kama Chama ina rekodi za kisiasa za kujivunia. Hii ni kupitia jitihada zake za kisiasa tangu mwaka 1992 na hata ulipofanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza baada ya kurudishwa mfumo wa Vyama Vingi, mwaka 1995.
Itakumbukwa pia, kuwa mwaka 2000, Chadema kama Chama, kilifanikiwa kuunda Serikali Kivuli kwa kuunda Baraza Kivuli la Mawaziri kupitia wabunge wake.
Chadema ilitoa pia Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Aidha, Chama hicho kimewahi kuwakaribisha vigogo wazito toka CCM, wote wakiwa wameshika nyadhifa za Uwaziri Mkuu.
Ni vigogo aina ya Marehemu Edward Lowasaa na Ndugu Fredrick Sumaye.
Lowassa na Sumaye, na kama ilivyotarajiwa na tulio wachambuzi, kwamba baada ya ‘ Ugomvi wa nyumbani’, wawili hao wangekuwa ni ‘ Wa kuondoka na Kurudi Nyumbani.’
Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, katika nyakati tofauti, wote wakarejea CCM.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.