Habari Kuu.
Serikali ya India chini ya Waziri Mkuu Narendra Modi imebadilisha jina la India na kuipa Nchi hiyo jina la “Bharat” katika kadi za mialiko ya chakula cha jioni zilizotumwa kwa wageni watakaohudhuria mkutano mkuu wa kilele cha G20 wiki hii na kuongeza uvumi kwamba nchi hiyo itabadilishwa jina rasmi hivi karibuni.
Rais wa India Droupadi Murmu alijitambulisha kama Rais wa “Bharat” badala ya “India “ katika kadi hizo zilizotumwa kwa Wageni wanaohudhuria mkutano wa G20.
India ni Mwenyeji wa Mkutano unaofanyika kila mwaka wa G20 likiwa ni kongamano baina ya Serikali zinazojumuisha Nchi 19 pamoja na Umoja wa Ulaya jijini New Delhi,Viongozi wengine Duniani akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Ufaransa Emanuel Macron watahudhuria.
Taifa hilo lenye zaidi ya watu bilioni 1.4 linajulikana rasmi kwa majina mawili ,India pamoja na Bharat lakini jina la India ndio hutumika zaidi ndani na nje ya mipaka ya nchi hiyo. “HINDUSTAN ” ni neno lingine linalotumika kuitambua nchi hiyo na mara kadhaa hutumwa katika fasihi na aina nyingine za tamaduni maarufu nchini humo.
Mapema hii leo vyombo vingi vya habari nchini India viliripoti kwamba Serikali inaweza kupeleka azimio la kubadilishwa kwa jina la nchi hiyo kutoka “India” na kuitwa “Bharat ” wakati wa kikao cha Bunge maalum mwezi huu.