Michezo
Nchini Uholanzi hapo jumapili kwenye mchezo kati ya Ajax na mtani wake wa jadi Feyenoord hali ilichafuka baada ya mashabiki wa Ajax kuzua vurugu zilizosababisha mchezo huo kusimamishwa.
Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki waliokuwa kwenye dimba la Johan Cruyff Arena. Vurugu zilianza tu baada ya Ajax kufungwa goli la 3 na Feyenoord ,ambapo mashabiki waliwasha fataki uwanjani hapo,hali iliozusha sintofahamu na mwamuzi kulazimika kusimamisha mchezo huo.
Pia, Askari wa farasi nao walilazimika kuwashughulikia mashabiki waliokuwa nje ya uwanja wakileta vurugu, huku timu yao ya Ajax ikiwa nyuma kwa mabao 3 na huku ikitajwa uharibifu kufanyika kwenye dimba hilo.
Mpaka sasa, Ajax inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa Ligi kuu Uholanzi, jambo ambalo mashabiki hawakulizoea kwa timu yao na huku msimu uliopita walipoteza Ubingwa wao wa Eredivisie kwa mahasimu wao ,timu ya Feyenoord Fc.
Kutokana na mwenendo mbovu wa timu hiyo ,menejimenti iliamua kumtimua Mkurugenzi wa michezo wa timu hiyo Sven Mislintat ambaye alichukua nafasi hiyo mapema mwezi Mei mwaka huu.