Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini ameomba radhi kwa taifa lake baada ya amri yake ya kutangaza sheria ya kijeshi kusababisha mtafaruku mkubwa na ukosoaji wa wazi dhidi ya uongozi wake. Katika hotuba fupi aliyoitoa Ijumaa, Yoon amesema anatambua athari za uamuzi huo na kuwaomba radhi raia wa Korea Kusini.
“Najua kuwa uamuzi wangu umesababisha mgawanyiko na mtafaruku nchini. Naomba radhi kwa kila mmoja na nawaomba mnisamehe,” amesema Yoon huku akiinamisha kichwa chake.
Rais huyo pia ametangaza kuwa anakiwachia chama chake tawala, People Power Party (PPP), kuamua hatima yake, akisema iwapo aendelee au kuachia madaraka ni juu yao kuamua.
Hotuba hiyo imekuja saa machache kabla ya Bunge la Korea Kusini kujadili hoja ya kutokuwa na imani naye. Vyama vya upinzani, vyenye viti 192 kati ya 300 katika Bunge, vinashinikiza kura hiyo huku wakisema tangazo la sheria ya kijeshi lilikuwa “kinyume cha katiba na mapinduzi haramu.”
Ili kufanikisha kumuondoa Yoon madarakani, upinzani unahitaji kura nane pekee kutoka kwa wabunge wa chama tawala.
Kiongozi wa chama tawala, Han Dong-hoon, amesema kuwa kujiuzulu kwa Rais Yoon ni jambo lisiloepukika. Dong-hoon amemtuhumu Rais Yoon kwa kuchukua hatua ya kutisha kwa kutangaza amri ya kijeshi na kudai kuwa rais huyo ameamuru maafisa wa ujasusi kuwakamata viongozi wakuu wa kisiasa kwa madai ya kula njama dhidi ya serikali.
“Rais Yoon ameamuru kamanda wa ujasusi kuwakamata viongozi wa kisiasa kama sehemu ya utekelezaji wa sheria ya kijeshi. Hili halikubaliki kabisa,” amesema Han Dong-hoon, akiongeza kuwa hatua zaidi za hatari zinaweza kuchukuliwa ikiwa Rais Yoon ataendelea kuwa madarakani.
Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imemsimamisha kazi kamanda wa ujasusi, Yeo In-hyung, ambaye amehusishwa na mpango wa kuwakamata viongozi wa kisiasa. Maafisa wengine wawili wa kijeshi, wakiwemo kamanda wa kamandi maalumu wa vita, pia wamesimamishwa kazi. Aidha, mwendesha mashtaka wa Korea Kusini ametoa amri ya kutosafiri nje ya nchi kwa maafisa kadhaa wa jeshi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi amekanusha madai kwamba alipokea maagizo yoyote kutoka kwa Rais Yoon kuhusu kuwakamata viongozi hao wa kisiasa.
Vyama vya upinzani vinashikilia msimamo wao wa kumuondoa Rais Yoon, wakitaja tangazo lake la kijeshi kuwa ni kitendo cha kukiuka katiba. Wafuasi wa upinzani walikusanyika kwenye majengo ya Bunge, wakiwa na mabango wakimtaka Rais Yoon aachie madaraka mara moja.
Jaribio la Rais Yoon kutangaza sheria ya kijeshi limesababisha taharuki kubwa nchini, pamoja na masoko ya fedha na washirika wa Korea Kusini. Hatua hiyo, hata hivyo, ilitenguliwa baada ya bunge kupitisha haraka sheria ya kuzuia tangazo hilo.
Hatima ya Rais Yoon inategemea kura ya kutokuwa na imani itakayopigwa Jumamosi, ambapo wabunge wa chama chake tawala wanahitajika kuamua ikiwa watamuunga mkono au kujiunga na upinzani.