Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga limefanikiwa kuwakamata watu watano kwa makosa ya wizi kwa njia ya mtandao ambao ni Said Amiri (21) mkazi wa Kimara Dar es Salaam, Athumani Amiri Athumani (24) mkazi wa Mbezi mwisho Dar es Salaam, Brayan Matina Mayunga (26) mkazi wa Mombasa Ukonga Dar es Salaam, Wakala, James John Nathaniel (24) mkazi wa Kitunda Dar es Salaam na Peter Michael Babuya (20) mkazi wa Arusha, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Taarifa iliyotolewa tarehe 19 Desemba, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi imeeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo jijini Dar es Salaam na Masasi mkoani Mtwara baada ya kujifanya mawakala wa kujitegemea (freelancers) wa kampuni za Tigo, Vodacom na Airtel na kuiba fedha kiasi cha Shilingi 20,390,000 kwa njia ya mtandao mali ya Abdul Hemed Shedafa, mfanyabiashara na mkazi wa wilaya ya Muheza mkoani Tanga.
Aidha, amesema baada ya uchunguzi wa kitaalam kufanyika imebainika kuwa walitumia mbinu za ulaghai, ikiwemo kutumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina mengine ili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.