Serikali ya Albania imetangaza kufungia mtandao wa TikTok kutoa huduma Nchini humo kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kutokea kwa tukio la kuuawa kwa Mtoto wa miaka 14 mwezi uliopita kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni ugomvi ambao ulianzia kwenye mtandao huo kati yake na Mwanafunzi mwenzie.
Waziri Mkuu wa Nchi hiyo Edi Rama baada ya kukutana na Wawakilishi wa Wazazi na Walimu kujadiliana kuhusu mustakabali wa Vijana na matumizi ya mitandao, amenukuliwa akieleza yafuatayo “kwa mwaka mmoja tutaifunga TikTok kabisa kwa kila Mtu, hakutokuwa na TikTok Nchini Albania”
Waziri Mkuu, Rama amesema marufuku hiyo ni sehemu ya mpango wa Kitaifa wa kuongeza usalama mashuleni na inatarajïiwa kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 2025.
Hata hivyo Uongozi wa Mtandao wa TikTok umekanusha kuhusika moja kwa moja na mauaji ya Kijana huyo ukisema kuwa hakuna ushahidi wowote kwamba Wahusika walikuwa na akaunti kwenye mtandao wao.
Hadi sasa Mataifa kama Ufaransa, Ujerumani na Ubelgiji tayari yameweka vizuizi kwa matumizi ya mitandao ya Kijamii kwa Watoto ambapo November 2024 Australia nayo iliidhinisha sheria kali zaidi ya kupiga marufuku kabisa matumizi ya mitandao ya kijamii kwa Watoto chini ya miaka 16.