HABARI KUU
Tanzania na Misri zimekubaliana kushirikiana katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja ili kuchochea ukuaji wa uchumi katika mataifa hayo mawili.
Akizungumza katika kikao kazi cha kimkakati kati ya Tanzania na Misri, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema ushirikiano huo utalenga pia miundombinu ya kimkakati ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabari wa barabara ya kutoka Cairo nchini Misri kupita Tanzani hadi Cape Town, Afrika Kusini. Kikao pia kilimhusisha Waziri wa Uchukuzi wa Misri, L.G Kamel Alwazeer.
“Tumekubaliana kukaa pamoja kuona namna ya kushirikiana kukarabati kwa viwango vya hali ya juu mtandao wa barabara ambao unaunganisha Afrika kutoka Misri mpaka Afrika Kusini. Nchini kwetu, sehemu ya barabara hiyo inaanzia Mkoa wa Songwe kutokea Zambia kupita Mbeya – Dodoma – Arusha kuelekea Namanga mpakani mwa Kenya na Tanzania,” amesema Bashungwa.
Bashungwa ameweka msisitizo wa mchakato huo kufanyika kwa haraka ili barabara hiyo iweze kuchochea ukuaji wa uchumi katika mataifa inakopitia.
Amesema wamekubaliana pia kushirikiana katika kubadilishana uzoefu wa kitaalamu kwa wanafunzi wanaohitimu taaluma ya uhandisi na ukandarasi katika vyuo mbalimbali kupitia mpango wa mafunzo kwa vitendo (SEAP), baina ya mataifa hayo mawili.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Bashungwa ameuelekeza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha miradi ya barabara ambayo itatekelezwa kupitia mikataba, kuwe na vipengele vya kumlazimisha mkandarasi kuwachukua wahitimu wa ukandarasi na uhandisi katika kusimamia miradi ili kujenga uzoefu wa kitaalamu.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi wa Misri, Alwazeer amesema Misri itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wa mataifa hayo ikiwemo kuunganisha Tanzania na Misri kupitia barabara inayokwenda hadi Afrika Kusini.