HABARI KUU
Waziri Mkuu wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amekutana na Waziri wa Nchi Kilimo na Mifugo wa Rwanda kujadili na kuweka sawa mikakati ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata maziwa jijini Mwanza.
Waziri Makamba amesema uwepo wa Kiwanda hicho cha Maziwa Jijini Mwanza kitatoa soko la maziwa na kuhamasisha wafugaji kufuga kwa namna ambayo mifugo yao itatoa maziwa mengi, tayari juhudi za Serikali zimeshaanza ili kukiwezesha kiwanda hicho kupata maziwa mengi zaidi ukizingatia Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na mifugo mingi zaidi Afrika.
Aidha, katika majadiliano hayo viongozi hao wawili wamejadili kuboresha na kuongeza uzalishaji wa nafaka kwa Watanzania na kuongeza uingizaji wa bidhaa hizo nchini Rwanda ambapo katika bidhaa za chakula huagiza mchele mwingi kutoka Tanzania.
Hati ya Makubaliano ya kujengwa kwa kiwanda hicho cha maziwa Misungwi Jijini Mwanza, ilisainiwa mapema mwezi Januari mwaka huu kati ya Serikali ya Tanzania na wawekezaji wa Rwanda.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba bado yuko kwenye ziara ya Kikazi ya siku tatu Nchini Rwanda.