HABARI KUU
Mgogoro katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umechukua mkondo wa kisheria baada ya Kinshasa kuishtaki Kigali katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ) jijini Arusha.
Kinshasa inadai kuwa Kigali imekiuka uhuru wa ardhi ya DRC na inaituhumu kwa kusaidia vita katika eneo hilo.
Katika maombi yake, DRC imeomba Rwanda kuzuiliwa kukiuka ardhi yake na kuondoa wanajeshi wake kutoka katika eneo ambalo inadai kuwa ni lao. Pia, DRC inataka mahakama itoe tamko kwamba vitendo vya Rwanda vimekiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu uadilifu wa ardhi.
Mbali na hilo, DRC inailaumu Rwanda kwa kutoa msaada kwa kundi la waasi la M23, ambalo linatuhumiwa kwa uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu ikidai kuwa msaada huo unakiuka pia mkataba wa EAC.