HABARI KUU
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imewataka watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanaotaka kuajiriwa na Kampuni ya DP World kujitokeza kuorodhesha majina kabla ya Machi 29, 2024.
TPA imesema katika mchakato wa uwekezaji bandarini hapo, “hakuna mtu yeyote atakayepoteza kazi.”
Machi 20, 2024, TPA ilitoa tangazo kwa watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam ikielezea mkataba walioingia na DP World ya Dubai unaohusu uendeshaji wa gati namba 0-3 na gati 4-7 kwa kipindi cha miaka 30.
Oktoba 22, 2023, TPA na DP World zilisaini mikataba mitatu mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Dodoma inayohusu uwekezaji na uendeshaji Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi.
Kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA). Mikataba hiyo ni wa nchi mwenyeji (HGA), wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.
Katika tangazo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenda kwa watumishi wa bandari, amesema kutokana na makubaliano yanayohusisha usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanapaswa kuchagua kati ya kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World.