NYOTA WETU
Mwanamuziki Zuhura Othman (Zuchu) ameandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kuwa na video moja iliyofikisha idadi ya watazamaji milioni 100 katika mtandao wa YouTube kupitia wimbo wa Sukari.
Kabla ya hapo hakuna msanii yeyote binafsi ‘solo’ aliyewahi kutoa video iliyofikia mafanikio hayo kwa Tanzania na Afrika Mashariki maana video zote nchini zilizofanya hivyo, ni zile ambazo wasanii wameshirikiana.
Sukari ni wimbo alioimba Zuchu akiuachia miaka mitatu iliyopita huku Trone na Laizer wakiwa ndiyo watayarishaji.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zuchu ameonesha kufurahia mafanikio hayo huku akieleza kuwa Sukari ndiyo wimbo uliobadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa.
Hata hivyo hakuacha kutoa shukrani kwa mashabiki wake pamoja na waliohusika katika maandalizi ya wimbo huo.
“Trone hongera sana kwa kuwa mtayarishaji wa wimbo wenye historia kubwa kwenye tasnia. Huu mwaka bado hatujauanza naamini ndani yako na kuna makubwa mengi watayashuhudia kupita collaboration zetu. Lizer kaka wimbo usingekamilika bila mchango wako wa mwendo na mixing kali asante sana kaka”. Ameandika Zuchu.
Ikumbukwe kuwa historia kama hiyo imewahi kuandikwa na mwanamuziki kutoka Nigeria Yemi Alade, mwaka Huu ndiyo mtego uliomnasa Yemi Alade, tangu video yake, Johnny (2014) kufikisha ‘views’ milioni 100 YouTube hapo Januari 2019 na kuandika rekodi kama msanii wa kwanza kike Afrika kufanya hivyo, hadi leo hajaweza kuwa na wimbo uliopata namba hizo.
Hadi sasa video za Bongo Fleva zenye ‘views’ zaidi ya milioni 100 YouTube ni Yope Remix (2019) – Diamond Platnumz ft. Innoss’B, Inama (2019) – Diamond ft. Fally Ipupa, Waah! (2020) – Diamond ft. Koffi Olomide, na Kwangwaru (2018) – Harmonize ft. Diamond.