HABARI KUU
Mohamed Omary, mkazi wa wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro anayedaiwa kumuua mke wake na kumzika ndani ya nyumba walimokuwa wakiishi amefikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro na kusomewa mashtaka manne.
Mashtaka hayo ni mauaji, udhalilishaji na ukatili anaodaiwa pia kuufanya kwa watoto wawili wa marehemu wenye umri wa miaka 12 na tisa.
Imedaiwa mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti ambapo katika Kesi ya kwanza namba 81008 ya mwaka 2024 Omary anadaiwa Januari Mosi 2024 alimuua Beatrice Ngongokwa na kumzika ndani ambapo hakutakiwa kujibu chochote kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.
Kesi ya pili namba 8101 ya mwaka 2024 inadaiwa kwa nyakati tofauti mtuhumiwa alifanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kuanzia April 2023 hadi Machi 2024 ambapo alimjeruhi mtoto wa marehemu kwa kumng’oa meno mawili, kumchoma moto sehemu za mapajani kwa kutumia kitu chenye moto, kumchoma na misumari na kumpiga rungu kichwani.
Kosa la tatu ni namba 1112 /2024 la udhalilishaji ambapo mtuhumiwa anadaiwa kulitenda kwa mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka 12.
Kosa la nne ni la ukatili wa kijinsia namba 8013 ambapo mtuhumiwa anadaiwa kulifanya kwa mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka tisa kwa kumng’oa meno, kumchoma mdomo na makalio, kumtengua jointi za mkono wa kushoto, na kumtoboa na misumari sehemu za siri.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo manne mtuhumiwa huyo alikana makosa matatu na kukiri moja la mauaji.
Kesi hiyo ya inatarajiwa kusomwa tena Machi 28, 2024.
Related Posts 📫
Discover more from JUNIITV.ONLINE
Subscribe to get the latest posts sent to your email.