HABARI KUU
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Paul Makonda, amewataka wale aliowaita Wanasiasa uchwara wanaojipendekeza kwa Rais Samia kwa kumtenganisha na Mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuacha mara moja tabia hiyo kwakuwa Viongozi hao wote ni kitu kimoja na hauwezi kuwatenganisha.
Akiongea Jijini Dar es salaam leo wakati wa mapokezi ya ndege mpya ya Air Tanzania, Makonda amesema “Mh. RC Chalamila hapa amenifurahisha kwelikweli, kuna kasumba ya ujinga unaoendelea wa kutaka kumtofautisha Dkt. Samia na Dkt. Magufuli, huwezi kuwatenganisha hao Watu na Viongozi wengi Wanafiki wanaotafuta kujipendekeza kwa Dkt. Samia kila wakipata jukwaa wanataka kumfanya kama Dkt. Samia sio sehemu ya Dkt. Magufuli”
“Kama Msemaji wa Chama (CCM) kila anachokifanya Dkt. Samia ndicho ambacho alikifanya Dkt. Magufuli na Watu hawa walisimama wakazunguka katika Taifa hili wakatafuta kura kwa pamoja huwezi kuwatenganisha na Waziri Mkuu wao yule pale Kassim Majaliwa, ningetamani leo iwe ni siku ya mwisho ya unafiki wa Viongozi na Wanasiasa uchwara wanaopambana kuwatenganisha Viongozi hawa, mafanikio haya tunayasherehekea wote kwasababu Chama ni kimoja, Serikali ni ya CCM na nyinyi Wananchi mliipigia kura”